************
Taasisi ya Hakimiliki Tanzania yatoa elimu kwa Watayarishaji wa kazi za Muziki nchini (Music Producers) na kuwaeleza umuhimu wa kusajili midundo (beats) ya kazi wanazoziandaa pamoja na umuhimu wa kuwa na makubaliano na msanii wakati wa utayarishaji wa kazi.
Kikao hicho kilichokuwa kimeandaliwa Tanzania Producers and Composers Association (TPCA) kimefanyika leo Februari 03, 2022 Jijini Dar es Salaam, ambapo lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutoa elimu ya Hakimiliki na kufafanua kwanini katika mgao wa mirabaha uliyofanyika hivi karibuni wengi wao hawajanufaika.
Akizungumza katika kikao hicho Mwanasheria wa COSOTA Lupakisyo Mwambinga alisisitiza kuwa COSOTA inatambua kuwepo na changamoto ya kukosekana kwa elimu ya Hakimiliki kwa wadau wengi wa sekta ya ubunifu na hivyo inaendelea kuweka juhudi ya kutoa elimu katika majukwaa tofauti kama vyombo vya habari na mitandaoni.
Nae Mwenyekiti wa TPCA Paul Matthysse (PFunk Majani) aliiomba COSOTA kushirikiana na chama hicho kuandaa fomu itakayokuwa inajazwa na msanii studio kabla ya kuachukua kazi yake (release form), fomu hiyo itakuwa ikionyesha makubaliano yao prodyuza na msanii na wakati wa usajili wa kazi COSOTA msanii alazimika kuwasilisha fomu hiyo kama sehemu ya kiambatanisho cha taarifa zake.
Pamoja na hayo Maprodyuza hao waliipongeza COSOTA kwa kuweza kuwapati elimu na wameahidi kushirikiana kwa karibu taasisi hiyo ili kuweza kusaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya Sanaa ili kila mbunifu aweze kunufaika.
Halikadhalika COSOTA imesisitiza kufanya marekebisho ya fomu ya usajili wa kazi za Muziki ili kuweza kuongeza vipengele vitakavyoonesha Hakishiriki vizuri.
0 Comments