Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AMUAGIZA RC HAPI KUVUNJA MKATABA NA MKANDARASI ANAEJENGA BARABARA YA MAKUTANO HADI SANZATE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia Wananchi wa Mkoa wa Mara katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ‘Kwangwa’ leo tarehe 06 Februari, 2022 mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi pamoja na huduma za afya zitolewazo hospitalini hapo.

************************

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Salum Hapi kuvunja mkataba na Mkandarasi anaejenga barabara ya Makutano hadi Sanzate Mkoani Mara.

Mhe. Rais Samia ametoa agizo hilo leo tarehe 06 Februari, 2022 wakati akihutubia wananchi wa Kwangwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kwangwa, Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo eneo hilo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Mkandarasi huyo ameshindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 50 ambayo imeanza kujengwa tangu mwaka 2013 ambayo itagharimu shilingi bilioni 54.5 itakapokamilika pamoja na barabara ya Musoma -Makoja yenye urefu wa kilomita 5 ambayo ilianza kujengwa mwaka 2020 inayogharimu shilingi bilioni 8.2.

Mhe. Rais Samia ameagiza uongozi wa mkoa wa Mara kutafuta wakandarasi wenye uwezo wa kifedha na mitambo katika kutekeleza miradi ya maendeleo mkoani humo.

Kwa upande mwingine Mhe. Rais Samia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mara kuwasimamisha kazi Wakuu wa Idara za Fedha, Idara ya Mipango na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi wa baadhi ya Halmashauri za mkoa huo kufuatia ubadhirifu wa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mhe. Rais Samia amewataka viongozi mkoani Mara kuacha ubinafsi na kufuja fedha zinazoelekezwa katika miradi ya maendeleo ya wananchi wa mkoa huo na badala yake wajikite katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia, Mhe. Rais Samia ameagiza Kamati zilizokuwa zikisimamia miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa kupitia fedha za Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 ziendelee kufuatilia ujenzi wa vituo vya afya na miradi ya maji inayotekelezwa nchini kote.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali itatafuta fedha kwa ajili kujenga vyuo vya ufundi stadi katika kila mkoa nchini ili kutoa fursa kwa vijana kuweza kujiajiri wenyewe.

Awali, Mhe. Rais Samia ameweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji wa Mugango – Kiabakari – Butiama utakaogharimu shilingi bilioni 70.5 utakapokamilika katika kijiji cha Mugango kilichopo wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara.

Mhe. Rais Samia amesema dhamira ya Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani na kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ambapo tayari asilimia 75 ya fedha za mradi zimeshatolewa na mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2022 au mapema Januari, 2023.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameutaka uongozi wa mkoa wa Mara pamoja na Wizara ya Maji kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi anaejenga mradi huo wa maji ili ukamilike kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments