*************
· Tani 259,170 zakaguliwa
Imeelezwa kuwa, Jumla ya tani 259,170 za mbolea zilizoingizwa kutoka nje ya nchi zilikaguliwa na kuhakikisha kuwa mbolea wanayouziwa mkulima inakidhi viwango vya ubora ili kuleta tija katika shughuli za kilimo nchini.
Ukaguzi huo uliofanyika katikaia kipindi cha Julai hadi Disemba 2021 ni moja kati ya majukumu makubwa yanayofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA) ya kuhakikisha kuwa biashara ya mbolea nchini inakidhi matakwa ya viwango bya ubora wa mbolea.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Gerod Nganilevanu alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya taasisi hiyo katika kikao kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Nganilevanu alibainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2021 – Disemba 2021, Mamlaka imefanya ukaguzi katika mikoa 26 ambapo jumla ya wafanyabiashara 2,031 sawa na asilimia 129 ya lengo wamekaguliwa.
Ameeleza kuwa, katika kipindi cha Julai 2021 – Disemba 2021 jumla ya wafanyabiashara 2,031 walikaguliwa. Kati ya wafanyabiashara hao, 1,151 (57%) walikuwa na leseni hai, 194 (10%) walikuwa na leseni zilizoisha muda wake na 686 (33%) hawakuwa na leseni kabisa, hivyo Mamlaka ilihakikiisha wafanyabiashara hao wanapatiwa elimu na kasha kupewa leseni.
Aliendelea kueleza kuwa, kufuatia ukaguzi huo mamlaka ilibaini kuwa jumla ya wafanyabiashara 880 sawa na asilimia 43 ya wafanyabiashara wote waliokaguliwa kwa kipindi cha hicho walijihusisha na biashara ya mbolea bila kuwa na leseni.
Akielezea hatua zilizochukuliwa, Nganilevanu alisema mamlaka imewasaidia wafanyabiashara wote waliokuwa na viambatisho stahili kuingia kwenye Mfumo wa Kimtandao wa Mbolea (FIS), ambapo takribani wafanyabiashara 343 waliokuwa hawana leseni kwa kipindi cha robo ya kwanza na ya pili waliweza kupata leseni za usajili.
Pamoja na hayo, Nganilevanu alieleza kuwa katika kipindi cha Julai – Disemba 2021 wakaguzi wa mbolea walipokuwa wakifanya ukaguzi katika mikoa ya Arusha, Kigoma na Tabora walibaini uwepo wa mbolea tisa (9) za kimiminika sokoni ambazo hazikusajiliwa na mamlaka hiyo.
Alizitaja Mbolea hizo kuwa ni Mawenzi Ansil booster, New power Booster, Top max crop leader, Vita booster, Tanzanite, Max golden Bloomv Plus N, Mokusaku brix, Herbolive, Suber AGROFOLIAR (NPK 23:23:23+TE)
Kufuatia hali hiyo mamlaka iliziondoa sokoni Mbolea hizo wafanyabiashara kupewa amri ya kuacha kuuza (stop sale order) mbolea hizo.
Akihitimisha wasilisho lake, Nganilevanu alisema pamoja na hatua zilizochukuliwa kwa wafanyabiashara wanaokiuka matakwa ya kisheria ya utengenezaji na biashara ya mbolea, mamlaka imeandaa Mpangokazi kwa ajili ya kufuatilia wafanyabiashara wote waliobainika kufanya biashara kinyume na taratibu za sheria ya mbolea.
Hata hivyo, Mpangokazi huo umezingatia katika kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wote ambao hawana mafunzo na vyeti vya mafunzo ili waweze kukidhi kigezo cha kufanyiwa usajili.
0 Comments