**********************
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Bi.Mwantum Mgonja ametoa maagizo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo na watalaam wake kuchukua hatua mara moja ya kuyafunga maduka yote ya dawa yaliyokaguliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba [TMDA] na kukosa vigezo huku akiwataka wamiliki wote kufuata sheria za Nchi.
Bi Mwantum Mgonja ameyasema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Chakula na Dawa [CFDC] ya Halmashauri hiyo ya Mkuranga na Wawakilishi wa TMDA.
Ambapo katika kikao hicho alipokea ripoti ya ukaguzi uliofanywa na TMDA kwenye maduka ya dawa za binadamu na mifugo, ukaguzi uliofanyika Machi 14-18 mwaka huu na kukuta mapungu mbalimbali ikiwemo kukutwa na dawa zilizokwisha muda wake, huku mengine kutokuwa na watoa dawa waliopata mafunzo.
Bi. Mwantum Mgonja alibainisha kuwa, Wamiliki wa maduka ya dawa wanatakiwa kutambua suala la kufuata sheria sababu inajulikana iliuwe na duka la dawa sifa ni zipi.
"Nakuagiza Mganga Mkuu kuhakikisha ndani ya Halmashauri hii ya Mkuranga, maduka yote ambayo hayana vibali na hayataki kufuata taratibu, ambayo hayana kibali cha kuuza hizi dawa, yafungiwe haraka sana kuanzia sasa napotoa taarifa hii.
"Lakini kingine katika yale maduka, nimezuia maduka ya dawa ambayo yanauza yakiwa hayana watalaam, tunawaita 'Famasia', mtu anafungua duka lake la dawa lakini anaenda kuuza dawa kienyeji, yale maisha ni maisha hatarishi, tunahatarisha wananchi wa Wilaya hii ya Mkuranga lakini pia tunahatarisha maisha yetu sisi binafsi ambao ni wakazi wa hapa Mkuranga." Alisema Mkurugenzi huyo, Bi. Mwantum Mgonja.
Aliongeza kuwa;
"Rai yangu nataka kuona maduka yote yanawatalaamu ambao ndio wanaouza dawa,
Lakini la mwisho nimetoa maelekezo kwa Mganga Mkuu, kuhakikisha kwamba dawa zote zinazouzwa ni dawa ambazo zipo ndani ya muda, wapitie wakague yeye na watalaamu kwenye maduka haya ya madawa kuona dawa ambazo zimeisha muda wake wa matumizi 'expire date' na zitolewe katika maduka hayo." Alisema Bi Mwantum Mgonja.
Mkurugenzi huyo Bi. Mwantum Mgonja amesisitiza kwa wamiliki wa maduka hayo wafuate sheria zilizowekwa na nchi na kuzifuata kwani atahakikisha atapita mitaani kusimamia hilo.
"Nchi hii tunaishi kwa mujibu wa sheria kanuni na kufuata utaratibu wa Nchi. Unapokuwa unahitaji haki, timiza wajibu wako."
"Inasikitisha sana lakini mimi ni mtu wa kutembea sana huko kwenye 'field' nitakuwa nazunguka huko, sasa ninawaomba sana kwa kauli ya kawaida kabisa, tufuate utaratibu, tutimize wajibu ilituweze kuidai haki, tunahatarisha maisha yetu." alimalizia Bi. Mwantum Mgonja.
Nae, Meneja wa TMDA Kanda ya Mashariki Bw. Adonis Bitegeko anayesimamia mikoa ya Pwani, Tanga na Dar es Salaam, alisema kuwa katika kikao kazi hicho wameweza kugusa masuala ya msingi yaliyokasimiwa kwa Halmashauri za Wilaya pamoja na kutoa taarifa hizo za ukaguzi wa maduka ya maduka ya Dawa.
"Tumetoa elimu na pia kutoa taarifa tuliofanya Machi 14-18, mwaka huu
Lakini pia kuwapatia uelewa wa udhibiti wa bidhaa za tumbaku na kuwakumbushia majukumu yao yaliyokasimiwa kwa Halmashauri kukagua na kutoa vibali vya maduka ya dawa,
"Tunashukuru wenzetu wamepokea vizuri na Mkurugenzi wa Mkuranga Bi. Mwantum Mgonja ameahidi kuchukua hatua za haraka kwa mapungufu yote yaliyobainika." Alisema Bw. Adonis Bitegeko.
Aidha, aliwataka watumishi wa Serikali kuwa makini katika kulinda dawa na vifaa tiba za Serikali kwani dawa nyingi zinazokamatwa kwenye maduka binafsi zinatoka katika vituo vya Serikali ambapo amewataka watumishi wa Serikali kuwa makini na kuhakikisha hakuna bidhaa zozote za dawa kwenda pahala pasipostahili ilikuhakikisha Wananchi wanapata huduma iliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Zuberi Ndikilwa alipongeza TMDA kufanya ukaguzi ndani ya Wilaya hiyo ambapo imempa chachu ya ufanyaji wa kazi na kupokea maagizo hayo ya TMDA na Mkurugenzi wa Wilaya hiyo ya Mkuranga.
"Tumepokea kwa faraja kutoka TMDA kwa ukaguzi huu lakini pia nimepata faraja kwa ukaguzi wote wa maduka binafsi, hamna dawa yoyote ya Serikali katika maduka hayo, hii inaonesha udhibiti wa dawa za Serikali tunavyozisimamia.
Aidha, amesema kuwa, mapungufu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kutoka kwa vibali zoezi hilo lipo chini ya Mfamasia wa Wilaya na likikamilika watatoa vibali huku wale ambao hawajaendelea kukidhi vigezo kuchukua hatua za kufunga maduka yao.
"Kuna mapungufu ya maduka ya dawa ambayo hayana vibali, tunalishughulikia na Kuna vibali ambayo vipo kwenye mchakato na Bodi ya Phamasia, na ikikamilika tutawapa pia ili kuendelea kufanya biashara pasipo na utata wowote." Alisema Dkt. Ndikilwa.
Hata hivyo, aliwataka ambao hawaja fanyia uhakiki upya vibali vyao na wasio na vibali wanafanya biashara hiyo, kuyafunga mara moja maduka yao mpaka watakapokamilisha huku pia akiwataka wanaofuatilia vibali kwenda kwenye ofisi yake.
"Nasisitiza zoezi hili ni endelevu kwa Wilaya yetu ya Mkuranga na wenye maduka yote ya dawa ambayo hayana vibali naomba wafike kwa ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ilikuweza kupata vibali na kuweza kupata maelekezo yote muhimu ya uendeshaji maduka hayo Muhimu na Famasia.
Aidha, alisema kuwa, zoezi hilo ni la kawaida na wanafanya kila robo mwaka kuweza kuhakikisha wanafuata sheria za TMDA na Famasia nchini.
"Tunafanya zoezi kama hili kupitia Kamati ya Afya ya Wilaya ambapo pia tunashirikiana na wenzetu wa TMDA, ilikuhakikisha usalama wa dawa kwa wananchi wa Mkuranga." Alisema Dkt. Zuberi Ndikilwa.
Katika taarifa ya ukaguzi huo wa TMDA kwenye Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Mkuranga, ambapo jumla ya maeneo 45 yalikaguliwa huku Famasi za rejareja idadi yake 8, Maduka ya Dawa Muhimu (DLDM)33 na maduka ya dawa za Mifugo idadi yake 4.
"Kati ya Famasia 8, zilizokaguliwa, mbili hazikuwa na vibali vya Baraza la Famasia ikiwa ni sawa na asilimia 25, Maduka ya dawa muhimu 33 kati ya hayo, 30 hayakuwa na vibali vya Baraza la famasia ikiwa ni asilimia 90.0 huku maduka 4 ya dawa za mifugo, kati ya hayo 3 hayakuwa na vibali sawa na asilimia 70.
0 Comments