Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (katikati) akizungumza na madereva wanaosafirisha kemikali kuhusu umuhimu wa kuchoma chanjo ya kujikinga na maradhi ya Uviko -19 wakati akifungua mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali kwa madereva hao mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Joyce Njisya na kushoto ni Kaimu Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias (kushoto) akitoa cheti cha ushiriki kwa mmoja wa madereva wanaosafirisha kemikali baada ya kufunga mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali kwa madereva hao mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam.
*********************
Na Fatma Salum-GCLA
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amewahimiza madereva wanaosafirisha kemikali nchini pamoja na Watanzania wote kupata chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 ili kulinda afya zao na kuimarisha nguvukazi ya Taifa.
Dkt. Mafumiko ameyasema hayo mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya madereva wanaosafirisha kemikali yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki.
“Naunga mkono jitihada za Serikali yetu katika kukabiliana na ugonjwa wa Uviko-19 ulioenea kwenye nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania, hivyo ningependa niwasisitize na kuwahamasisha kuhusu kupata chanjo ya ugonjwa huo ambayo inatolewa bure na kwa hiyari katika vituo mbalimbali vya afya kote nchini,” alisema Dkt. Mafumiko.
Pia alibainisha kuwa chanjo hizo ni salama kwa kuwa zinapita kwenye vipimo na kuthibitishwa na wataalamu hivyo ni jambo jema watu wanapopata fursa ya kuchanja waichangamkie kwa sababu chanjo inasaidia kujikinga na maambukizi na hata ikitokea mtu ameambukizwa basi inamsaidia asizidiwe na maradhi hayo.
Akiwasisitiza madereva kuhusu kuzingatia kanuni za usalama katika kusafirisha kemikali, Dkt. Mafumiko alieleza kuwa pamoja na faida nyingi za kemikali katika maisha ya kila siku, ndani yake zimebeba hali hatarishi na zinaweza kuleta madhara makubwa kwa afya na mazingira kama zitatumika bila kuzingatia matumizi sahihi na usalama wakati wa uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi na matumizi mengine.
Akifunga mafunzo hayo Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias amewataka madereva hao kujiepusha na utumiaji wa vilevi na dawa za kulevya kwa kuwa jambo hilo ni hatari katika usafirishaji wa kemikali.
“Ni matarajio yangu kuwa, baada ya mafunzo haya mtaweza kuzingatia taratibu za usafirishaji salama wa kemikali kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani namba 3 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2020 katika nyanja zote. Aidha, mnategemewa kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha wadau na madereva wengi zaidi kupata mafunzo haya pamoja na kueneza elimu hii katika maeneo yenu ya kazi ili kulinda afya za watu, wanyama na mazingira,” alisema Elias.
Naye Kaimu Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki ya Mamlaka hiyo, Dastan Mkapa amewashukuru wamiliki wa magari yanayosafirisha kemikali kwa kuwapa fursa madereva wao kuhudhuria mafunzo hayo yenye tija katika kazi zao za kila siku.
Kwa upande wao madereva waliopatiwa mafunzo wameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwapa elimu ambayo itawasaidia kuepuka madhara kwenye kazi yao ya kusafirisha kemikali.
Mafunzo hayo ya siku mbili kwa madereva wanaosafirisha kemikali yalihudhuriwa na madereva zaidi ya 200 kutoka kampuni mbalimbali nchini ambao walipewa vyeti vya ushiriki wa mafunzo hayo.
0 Comments