Ticker

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI SINGIDA YAPANIA KUWAKOMBOA WENYE MAHITAJI MAALUM


Bweni jipya la Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum Shule ya Msingi Mchanganyiko Mgori likiwa kwenye hatua za mwisho kukamilika
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Mhe Elia Digha akieleza mafanikio ya halshamashauri yake.
Wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwa wakiwa darasani.

.......


Na Abby Nkungu, Singida


HALMASHAURI ya wilaya ya Singida imeweka mikakati ya kuboresha miundombinu na mazingira duni ya kujifunzia na kufundishia watoto wenye mahitaji maalum na tayari imejenga bweni la kisasa lenye thamani ya sh milioni 80 kwa ajili ya watoto hao.


Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Elia Digha alisema kujengwa kwa bweni hilo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 40 ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya miaka mitano iliyoanza mwaka huu wa fedha 2021/2022 hadi 2025/2026.


“Ujue hii Programu japo ni nzuri lakini wataalamu wetu hawajaifafanua vyema, ila sisi kwa kuanzia tumejikita zaidi kwenye elimu ya watoto wenye mahitaji maalum ambapo tumechukua Sh milioni 80 za UVIKO 19 na kujenga bweni zuri pale shule ya Msingi Mchanganyiko Mgori kwa ajili ya kundi hilo” alieleza Digha.


Alisema kuwa baada ya bweni hilo kukamilika watapeleka vitanda, magodoro na mahitaji mengine ya msingi kisha kwa kushirikiana na Serikali kuu watapeleka vifaa maalum vya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni vitabu, mashine maalum, miwani, vibao na vingine vingi sanjari na kuboresha miundombinu mingine ikiwemo vyoo kwa wasichana na wavulana.


“Kama halmashauri, tuna mkakati wa kuboresha elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum ambao utekelezaji wake unaenda pamoja na hii Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambapo sasa baada ya kumaliza suala la miundombinu na vifaa ndipo tutageukia kwenye suala la kupeleka walimu wenye taaluma ya kufundisha watoto hao” alisema.


Alieleza kuwa hivi sasa halmashauri hiyo ina jumla ya shule 31 zinazotoa elimu Jumuishi kwa watoto wenye mahitaji maalum lakini zenye nafuu ya mazingira ni mbili tu; nazo ni Mtinko na Mgori na mpango uliopo ni kuwakusanya wanafunzi wengine kuwapeleka kwenye shule hizo zenye mabweni.
Mwalimu wa Kitengo cha Elimu Maalum katika shule ya msingi Mchanganyiko Mgori, Hemed Kilango alisema kujengwa kwa bweni hilo katika shule hiyo ni mwanzo mzuri wa kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum ili nao wapate haki ya elimu kama watoto wengine wa kawaida.


"Kwa kweli tunashukuru kwa hatua hii ya bweni ingawa bado kuna uhaba wa walimu wenye utaalamu wa lugha ya alama, ukosefu wa miundombinu rafiki na zana za kujifunzia na kufundishia wakati bajeti yao ni ndogo haitoshi kununulia hata kofia, miwani ya jua au mafuta ya ngozi kwa wanafunzi wenye ualbino” alifafanua.


Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Amiri Mohamed pamoja na kushukuru kujengewa bweni alisema bado kuna haja ya kuwepo vifaa muhimu vya kujifunzia na kufundishia kama vile Mashine na vitabu vyenye maandishi ya nukta nundu na karatasi maalum kwa ajili ya kuchorea.


“Mimi nina uoni hafifu lakini wapo wenzetu ambao hawaoni kabisa wanategemea hisani ya wenzao wanaoona kuwasomea maandishi ya kawaida ubaoni ndipo waweze kuandika kwenye vibao vyao na hata mtihani unaletwa kwa maandishi ya kawaida kwa wote sisi wenye mahitaji maalum na wenzetu wanaoona. Sasa sisi mpaka mwenzio akusomee ndipo uandike” alieleza kwa masikitiko.


Taarifa za idara ya elimu katika halmashauri hiyo inaonesha kuwa pamoja na uhaba wa vifaa, pia walimu 20 wa elimu maalum wanahitajika kwani waliopo ni sita tu, wawili kati yao ni wa lugha ya alama jambo ambalo Ofisa elimu maalum, Elihuruma Funda alisema linatafutiwa ufumbuzi.


Naye mmoja wa wazazi, Neema Dule alisema kuwa ni vyema Serikali ikaharakisha mchakato wa kuboresha shule hizo ili kuwavutia wazazi na walezi kuwasomesha watoto wenye ulemavu badala ya kuwaficha majumbani, hali inayowanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, watoto wenye ulemavu wanaoandikishwa kuanza Darasa la Kwanza katika shule mbalimbali Nchini ni chini ya asilimia moja hali inayoathiri suala la ukuaji wao kimwili, kiakili kihisia na kijamii.

Post a Comment

0 Comments