************************
NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mwanaidi Ali Khamisi amewataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki Sensa ya watu na Makazi ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya kimaendeleo.
Aidha amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake ya kuwaamini wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi huku akiwataka wanawake hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii kwa lengo la kumsaidia Rais ili aweze kutimia majukumu ya kulijenga Taifa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwanaidi alisema kimsingi Sensa ya watu na makazi inapaswa kuungwa mkono na wananchi wote kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
"Nawasihi wanawake wenzangu kuona umuhimu wa kushiriki katika sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu, kimsingi zoezi hili ni muhimu kutokana na faida zake hasa linapokuja suala la maendeleo ya nchi" alisema Mwanaidi
Aidha kuelekea katika kilele cha siku ya wanawake Duniani Machi 8 Mwaka huu, yenye kaulimbiu isemayo ' Kizazi chenye haki ya usawa kwa Maendeleo Endelevu, tujitokeze kwa wingi siku ya kuhesabiwa.
Naibu Waziri huyo alisema Tanzania inashuhudiwa ikiendelea kupiga hatua siku hadi siku chini ya Rais Samia.
0 Comments