Ticker

6/recent/ticker-posts

MKEMIA MKUU WA SERIKALI ASISITIZA UADILIFU NA UCHAPAKAZI KWA WATUMISHI

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko (aliyesimama) akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wajumbe wapya wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika katika ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Makao Makuu Jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 15 Machi, 2022. Wengine kutoka kulia ni Mjumbe wa Kamati, David Elias, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Evaclotida Kapinga na Mwenyekiti wa Kamati mpya ya Uadilifu, Benny Mallya.


Wajumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka na Wawezeshaji wa mafunzo ya kamati hiyo wakimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya siku mbili yanayofanyika katika ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakiwa kwenye mafunzo ya maadili ya utendaji yanayofanyika katika ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali leo Jijini Dar es Salaam.


Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko (wa pili kushoto, waliokaa) akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Uadilifu ya Mamlaka na Wawezeshaji wa mafunzo ya kamati hiyo baada ya kufungua mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika katika ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam.

************************

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amewasisitiza wajumbe wa Kamati mpya ya Uadilifu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kufanya kazi kwa uaminifu na weledi ili kusaidia watumishi wa Mamlaka kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uzalendo na kufikia viwango vinavyotarajiwa.

Dkt. Mafumiko ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya kamati hiyo kuhusu Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma yanayofanyika kwa siku mbili katika ofisi ya Makao Makuu ya Mamlaka jijini Dar es Salaam.

“Majukumu mengi ya Mamlaka hii ni nyeti hivyo Kamati ya Uadilifu ni muhimu kwa sababu ina nafasi kubwa katika kuhakikisha watumishi wanazingatia uaminifu na uadilifu kwenye kazi zao za kila siku. Ni imani yangu kuwa kupitia kamati hii kila mtumishi atafanya kazi kwa uzalendo, utii, uadilifu na umahiri akijua kwamba anafanya kazi ambayo mwisho wa siku inapelekea maamuzi ya kisheria ambayo yanaweza kuleta athari ya moja kwa moja kwa mtu binafsi au kwa taifa,” alisisitiza Dkt. Mafumiko.

Pia alieleza kuwa Mamlaka imeandaa mafunzo ya kamati hiyo ili kuwapatia wajumbe misingi ya utekelezaji wa majukumu yao kimaarifa, kisheria, kiujuzi na kimtizamo ili kuendelea kujenga taswira nzuri ya taasisi kwa wadau na hata kwa Serikali ambayo ndiyo mdau mkuu.

Aidha alitoa rai kwa wajumbe wa kamati hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kujali haki na uaminifu na kuhakikisha kila mtumishi anafanya kazi kwa ufanisi na uadilifu kwa maslahi ya taasisi na taifa kwa ujumla kwa sababu huo ndio msingi wa mafanikio katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka na suala hilo linapewa kipaumbele kikubwa na Mamlaka hiyo.

“Kamati hii ina jukumu kubwa la kuainisha viashiria vya uvunjifu wa maadili na kuwashauri watumishi kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vinayoweza kusababisha uvunjifu wa maadili lakini pia ina jukumu la kumshauri Mtendaji Mkuu na kumpa mapendekezo ya kukuza maadili katika taasisi hii,” alisema Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Steven Agwanda alisema kuwa kamati hiyo ili ifanye kazi kwa ufanisi inatarajia ushirikiano kutoka kwa Menejimenti ya taasisi ambao ndio watoa maamuzi hivyo basi Menejimenti nayo ina nafasi kubwa katika kuhakikisha kamati hiyo inafanya kazi zake vizuri.

Kamati mpya ya Uadilifu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeundwa baada ya iliyokuwepo awali kumaliza muda wake na inatarajiwa kufanya kazi kwa muda wa miaka mitatu.

Post a Comment

0 Comments