Ticker

6/recent/ticker-posts

MKUU WA WILAYA NAMTUMBO AMHAKIKISHIA JAJI MKUU USHIRIKIANO

Na Innocent Kansha – Mahakama, Songea

Mkuu wa Wilaya ya Namtubo, Dkt. Julius Ningu leo tarehe 1 Machi, 2022 amesisitiza kuwa ataendelea kutenda haki kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, hasa katika nyanja ya kuendeleza utamaduni wa kutenda haki kwa wananchi.

Ameyasema hayo alipokutana na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake alipomtembelea akiwa katika ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Songea.

“Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imekuwa imara katika kuendelea kutoa ushirikianao wa karibu na Mahakama ya Wilaya hususani maeneo yote ya kumsaidia mwananchi kufikia haki na endapo kunakuwa na jambo lolote huwa tunawasiliana kwa karibu kutatua changamoto kwa pamoja na haishangazi kuona mihimili yote inachapa kazi bega kwa bega,”alisema.

Akiongelea suala la ukiukaji wa haki za binadamu, Mkuu huyo wa Wilaya alitanabaisha kuwa hakuna ukiukwaji wa maadili kwa kiwango kikubwa katika Wilaya yake unaopelekea uvunjivu wa amani wa kutisha.

“Katika jamii yenye mchanganyiko wa tamaduni na desturi mbalimbali matukio ya ukiukwaji wa haki na masuala ya kujichukulia sheria mkononi halikwepeki, kwa uchache yanapojitokeza huchukua hatua stahiki mara moja ili kuthibiti hali hiyo,”alisema.

Aidha, Dkt. Ningu alisifia Mahakama ya Tanzania kwa mabadiliko makubwa iliyoyafanya ya kiuntendaji ambayo yamerejesha imani na taswila chanya kwa wananchi.

“Ni kweli Mahakama imebadilika sana, tunaweza kusema mfumo wake ni mfumo jumuishi wa kuwafanya wananchi waweze kuielewa Mahakama kwa sababu hapo awali ‘psychological space’ kati ya Mahakama na wananchi. Mtazamo aliokuwa nayo mwananchi ni kwamba ukienda mahakamani wewe ni kuhukumiwa, lakini kumbe ni kusikilizwa haki zake,”alisema.

Alibainisha kuwa mfumo ambao Mahakama ya Tanzania inaotumia hivi sasa ni nzuri, lakini mbinu inayotumika inabidi iboreshwe zaidi. Amesema kuwa kitu ambacho wamejaribu kupanga katika Wilaya yake ya Namtumbo wameamua kupitia vikao vyao kuiomba Mahakama ya Wilaya Namtumbo kuanza utekelezaji kwa kuanziasha klabu za sheria mashuleni ili kuwajengea uwezo wanafunzi kupitia elimu hiyo waweze kujua na kupata uelewa wa pamoja.

“Tunatafuta namna bora ya kuwafanya wananchi waielewe Mahakama kama chombo rafiki cha utoaji haki kwa wananchi, hii itaongeza pia kujenga imani chanya na kuepuka kuona Mahakama kama chombo kisichokuwa karibu na mwananchi,” alisema.

Mkuu huyo wa Wilaya alipendekeza Maafisa wa Mahakama pale inapowezekana wanaweza kutoa elimu kwenye mikutano ya hadhara inayoandaliwa na Ofisi yake ili kutatua changamo za ukosefu wa ufahamu wa mambo mbalimbali yanayomgusa mwananchi na majukumu ya msingi ya Mhimili.

“Maafisa wa Mahakama wanaweza pia kutumia matukio kama vile Mahafali ya shule za sekondari na Msingi kuelezea wajibu na haki alizonazo mwananchi na jinsi anavyoweza kuitumia Mahakama kupata haki hizo kwa wakati bila kucheleweshwa kwa namna yoyote,” alisema.

Kwa mujibu wa Dkt. Nungi, viongozi hao pia wanaweza kutumia hadhara kubwa inayokuja mahakamani kuwaelimisha wananchi nini wanapaswa kufanya kupitia Mahakama ili haki ionekane kutendeka wanapokuwa na mashauri mahakamani.

“Tutahakikisha tunatumia njia mbalimbali kupitia mikusanyiko halali ya wananchi kupenyeza elimu hata ya muda mfupi kuwajengea uwezo wananchi wazione Mahakama zetu ni rafiki na ni chombo cha haki na wala sio sehemu ya kuhukumiwa”, alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Mkuu wa Wilaya akatoa ushauri wa kutumia utaratibu wanaoutumia Shirika la Hifadhi ya wanyapori TANAPA la kutumia njia ya uwajibikaji wa kijamii “Corporate Responsibility” ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji wa elimu ya shughuli za Mahakama.

Baada ya mazungumzo hayo, Jaji Mkuu alielekea katika Mahamaka ya Wilaya ya Namtumbo kuzungumza na watumishi.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt. Julius Ningu Kitabu cha Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania Awamu ya pili 2021/2022 hadi 2024/2025, alipomtembelea Ofisini kwake, Leo tarehe 1 Machi 2022.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Namtumbo hawapo pichani wakati wa ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Leo tarehe 1 Machi 2022.



Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Namtumbo, Mhe. Gloria Lwomile akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo ichani) wakati wa ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama Wilayani Namtumbo



Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Namtumbo waliohudhuria kwenye kikao Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo ichani) wakati wa ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za Mahakama Wilayani Namtumbo

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akijadili jambo na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt. Julius Ningu wakati wa kwenda kukagua Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo lililokatika hatua za mwisho za kukamilika kwake.
Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo lililokatika hatua za mwisho za kukamilika kwake.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyenyoosha mkono) akijadili jambo na Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Moladi Limited wakati wa kukagua Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo lililokatika hatua za mwisho za kukamilika kwake.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Namtumbo wakati wa ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Sekela Moshi na Kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma

Picha na Innocent Kansha - Mahakama

Post a Comment

0 Comments