Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha na wadau wakikata keki maalum kwenye Jukwaa la Wanawake Shupavu Royal Connect 2026 – Lake Zone
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha akizungumza wakati wa Jukwaa la Wanawake Shupavu Royal Connect 2026 – Lake Zone.
**
Jukwaa la Wanawake Shupavu Royal Connect 2026 – Lake Zone limefanyika kwa mafanikio makubwa Juni 20, 2026 katika mji wa Bariadi, mkoani Simiyu, likiwakutanisha wanawake, viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiuongozi.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, huku Mgeni Maalum akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Edith Swebe.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na HolySmile Company Limited kupitia jukwaa la Wanawake Shupavu Royal Connect, ikiongozwa na kauli mbiu “Mwanamke Akisimama, Jamii Inasonga Mbele”, ililenga kutambua na kuthamini mchango wa wanawake pamoja na wadau mbalimbali wanaochangia maendeleo ya jamii katika sekta tofauti.
Katika usiku huo wa heshima na utambuzi, jumla ya tuzo saba zilitolewa kwa wanawake na wadau waliotoa mchango mkubwa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Miongoni mwa waliotunukiwa tuzo hizo ni ACP Edith Swebe kwa mchango wake katika kuimarisha usalama na ulinzi, pamoja na Salma Mipawa aliyepata tuzo kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya madini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Anamringi Macha amelipongeza jukwaa la Wanawake Shupavu Royal Connect kwa kuendelea kutoa hamasa kwa wanawake na kuwapa fursa ya kuonesha uwezo wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Amesema wanawake wana nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo ya familia, jamii na Taifa, hivyo ni muhimu kuendelea kuwawezesha, kuwatambua na kuwajengea mazingira yatakayowawezesha kufikia malengo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa HolySmile Company Limited na Mratibu Mkuu Jukwaa la Mwanamke Shupavu, Bw. Arnold Bweichum maarufu kama HolySmile, amesema jukwaa hilo ni programu endelevu inayolenga kutambua, kuhamasisha na kuwaunganisha wanawake wanaofanya kazi kubwa zenye matokeo chanya katika jamii.
Arnold Bweichum
Ameeleza kuwa kupitia Wanawake Shupavu Royal Connect, wanawake wanapata nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujenga mitandao ya ushirikiano na kufungua milango ya fursa mpya za maendeleo.
“Dhamira yetu ni kuendelea kuwainua wanawake wenye ushawishi chanya katika jamii kwa kutambua mchango wao na kuwahamasisha kufanya makubwa zaidi. Tunataka kujenga mtandao imara wa wanawake wa Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla,” amesema Bw. Bweichum.
Ameongeza kuwa waandaaji wamejipanga kuhakikisha jukwaa hilo linaendelea kufanyika kila mwaka ili kuibua na kutambua wanawake wanaofanya mambo makubwa katika jamii pamoja na kuimarisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.
Ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, wageni waalikwa, washiriki, wadhamini na wadau wote waliochangia kufanikisha tukio hilo ambalo limeendelea kuwa chachu ya maendeleo na uwezeshaji wa wanawake katika jamii.



































0 Comments