Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU KATIBU MKUU MAFURU AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA TRA

Naibu Katibu Mkuu-Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru (wa pili kushoto) akizindua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania leo 02/03/2022 mkoani Dodoma. Anayeshuhudia katikakati ni Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Alphayo Kidata na anayemfuatia ni Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Suzan Mgangwa.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakishuhudia uzinduzi rasmi wa Baraza hilo leo 02/03/2022 mkoani Dodoma.
***************************

Na Mwandishi wetu

Dodoma.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru amezindua Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwataka watumishi wa mamlaka hiyo kuweka mikakati itakayoiwezesha kukusanya mapato kwa ufanisi zaidi.

Uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika leo jijini Dodoma ni wa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996 ambapo Bw. Mafuru amekaribisha mawazo ya wadau hasa watumishi wa TRA ili waweze kusaidiana kutunga sera na sheria zitakazopelekea kuongezeka kwa makusanyo ya kodi.

“Ufanisi na utendaji wa Serikali unategemea kwa kiasi kikubwa utendaji wenu. Hivyo, ni vema mtambue kuwa, mmepewa majukumu muhimu na mmebeba dhamana kubwa ya kuiwezesha Serikali kuleta maendeleo katika nchi,” alisema Bw. Mafuru.

Aidha, amewataka wajumbe wa baraza hilo waliochaguliwa kutumia nafasi waliyoipata katika kuwaunganisha watumishi na viongozi wa mamlaka ili waonyeshe imani yao kwa watumishi hao.

“Ni imani yangu kuwa, ushiriki wenu kwenye baraza hili utakuwa na tija na utawezesha kutoa michango yenye kuleta tija na maendeleo ya mamlaka yetu na serikali kwa ujumla,” alieleza.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza hilo jipya la TRA amesema kwamba, wastani wa makusanyo kwa mwezi katika mwaka wa 1996/97 wakati mamlaka hiyo inaanzishwa, ulikua shilingi billioni 42 ambapo kwa sasa wastani wa makusanyo kwa mwezi ni shillingi trillioni 1.85.

“Mwezi Desemba, 2021 mamlaka imefanikiwa kukusanya shilingi trillioni 2.5, ikiwa ni kiwango ambacho ni cha juu zaidi ya makusanyo yote ya mwezi tangu Uhuru wa Taifa letu. Aidha, makusanyo ya mapato kutoka Zanzibar nayo yameimarika sana baada ya TRA kuchukua hatua kadhaa za kimkakati za kuongeza ufanisi,” alisema Bw. Kidata.

Bw. Kidata ameongeza kuwa, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Januari cha mwaka wa Fedha 2021/22, Mamlaka ya Mapato Tanzania imefanikiwa kukusanya kiasi cha shillingi trillioni 12.937 sawa na ufanisi wa asilimia 96.8 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 13.370.

“Kati ya kiasi hicho, makusanyo halisi kwa Tanzania Bara ni shillingi trillioni 12.743 sawa na ufanisi wa asilimia 97.0 kutoka kwenye lengo la kukusanya shillingi trillioni 13.136. Kwa upande wa Zanzibar makusanyo halisi yalifikia shillingi milioni 193,935.7 sawa na ufanisi wa asilimia 82.7 ukilinganisha na lengo la kukusanya shilingi milioni 234,573.9,” alisema Bw. Kidata.

Naye, Kamishna wa Kazi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bi. Suzan Mgangwa ameipongeza mamlaka hiyo kwa kuzindua baraza hilo linalowaweka pamoja watumishi wa TRA kote nchini ili kufanya majadiliano kuhusu utekelezaji wa mipango ya mamlaka kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi sehemu za kazi.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru amezindua baraza hilo la wafanyakazi wa TRA kwa niaba ya Naibu Waziri wa wizara hiyo Bw. Hamad Chande (Mb) ambapo watumishi takribani 400 wamehudhuria uzinduzi huo ulioambatana na uchaguzi wa viongozi na wajumbe wa baraza hilo.

Post a Comment

0 Comments