***********************
Na Zena Mohamed,Dodoma.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti Aya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amewaagiza waajiri wote wawasimamie Wakurugenzi au Wakuu wa Idara katika sehemu zinazosimamia Rasilimaliwatu katika taasisi zao kutumia mfumo wa kieletroniki wa tathimini ya hali ya watumishi katika utumishi wa umma na kuwataka wakamilishe zoezi hilo kabla Machi 31 mwaka huu.
Amesisitiza kuwa Taasisi ambazo hazitakamilisha zoezi hilo zitakuwa zimekiuka maelekezo ya Serikali na hatua stahiki zitachuliwa.
Waziri Mhagama amesema hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na wahabari na kuzindua mfumo huo ambapo amesema
Mfumo huo umesanifiwa na kujengwa kwa ajili ya kufanya tathmini ya hali ya Watumishi wa Umma kwa idadi, majukumu yao na vituo wanavyofanyia kazi.
"Wote tunajua kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina majukumu mengi ya Kisera na kiutendaji yanayotekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayolenga kuimarisha usimamizi wa Rasilimaliwatu tangu mtumishi anapoajiriwa mpaka atakapostaafu,
"Pia tunajua umuhimu wa Rasilimaliwatu katika kuzifanya rasilimali nyingine ziweze kuleta maendeleo nchini na nmekuwa nikisisitiza suala hili mara kadhaa kwamba bila kuisimamia vizuri Rasilimaliwatu basi hizo rasilimali nyingine zote tulizonazo haziwezi kutuletea maendeleo tunayokusudia,"amesema.
Amesema kuwa Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Hali ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma umesanifiwa na kujengwa na Wataalamu wa ndani ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo amesema jambo hilo ni la kujivunia kwa sababu bila hivyo Serikali ingeweza kuingia gharama kubwa katika kusanifu na kujenga Mfumo kama huo kwa kutumia Wataalamu au Washauri Waelekezi na pengine wa kutoka nje.
"Ni jukumu letu kutunza, kusimamia na kuulinda Mfumo huu ili uweze kufanya kazi iliyokusudiwa ipasavyo,"amesema.
Mhagama ameeleza kuwa mara baada ya kusanifiwa na kujengwa kwa Mfumo huo, Ofisi ya Rais - UTUMISHI iliupeleka kwa Waajiri wote waliopo kwenye Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara katika Utumishi wa Umma (HCMIS) ili kuingiza taarifa na takwimu sahihi kuhusu idadi na mgawanyo wa watumishi kulingana na huduma zinazotolewa na taasisi za Umma.
Ambapo amesema kwa taasisi zilizo nje ya Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara katika Utumishi wa Umma (HCMIS) zilipelekewa nyenzo ya kukusanya taarifa ambazo zitaingizwa kwenye Mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kuchakatwa zaidi.
" Na Mfumo tunaozindua leo unalenga kutuwezesha kukusanya, kuchakata na kuchambua taarifa za Watumishi kwa njia ya kisayansi ili kubaini mahitaji halisi ya Watumishi katika Wizara na Taasisi za Umma,
"Zoezi hili litatusaidia katika kutathmini hali halisi ya Watumishi waliopo na wanaohitajika katika taasisi zote za umma ili kuweza kuwapanga kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kila taasisi na kwa kufanya hivyo, Serikali itakuwa na taarifa na takwimu sahihi kuhusu watumishi waliopo, mahitaji ya watumishi wanaohitajika katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wananchi,"ameeleza Mhagama.
Aidha amesema matarajio ya zoezi hilo ni kuweka msawazisho wa Watumishi wa Umma katika taasisi za Umma kwa tathmini iliyopo inabainisha kuwa utoshelevu wa mahitaji ya watumishi kwa taasisi za Umma upo kati ya asilimia 52 hadi 90.
Amesema zoezi hilo lilianza mwezi Januari mwaka huu na lilitakiwa likamilike katikati ya mwezi Februari, mwaka huu hata hivyo amesema wataangalia mwenendo wa zoezi hilo kwasababu mpaka leo inaonesha bado Wizara na Taasisi nyingi hazijakamilisha zoezi hilo.
"Kwa taarifa tulizo nazo mpaka leo kati ya Wizara na Taasisi 427 zilizo kwenye Mfumo wa HCMIS zote zimeshaanza kutumia Mfumo na zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa zoezi hili na zipo kati ya asilimia 13 hadi 97,"amesema.
Aidha amesema taasisi 41 kati ya taasisi 70 zilizo nje ya Mfumo wa HCMIS zimeshawasilisha taarifa zao na sasa wataalam wanachakata taarifa hizo kwa ajili ya kuziweka kwenye Mfumo.
"Hata hivyo bado kuna Wizara na Taasisi nyingi hazijatekeleza maelekezo ya Serikali ipasavyo hivyo tunaomba viongozi wa taasisi wawajibike ipasavyo ili tuweze kufikia lengo la zoezi hili muhimu litakaloimarisha usimamizi wa Rasilimaliwatu,"amesema.
0 Comments