Ticker

6/recent/ticker-posts

RUKWA KUONDOKANA NA MGAO WA UMEME- ENG. MARO

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Ndugu Rainer Lukala (katikati) akizungumza jana wakati wa ziara ya Kamati ya Usalama Mkoa kukagua kituo cha kupoza umeme mjini Sumbawanga ambapo serikali imekamilisha mradi wa kujenga tranfoma mpya yenye uwezo wa megawati 15 pamoja na njia nne za kusambaza umeme.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa TANESCO Rukwa jana wakati wa ziara ya Kamati ya Usalama Mkoa kukagua kituo cha kupoza umeme Sumbawanga ambapo mradi mpya wa kuboresha umeme Sumbawanga umekamilika hatua itakyondoa mgao wa umeme Rukwa na wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi. Meneja wa Tanesco mkoa wa Rukwa Mhandisi Fanuel Maro (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa Kamati ya Usalama Mkoa wa Rukwa kuhusu mradi wa kuboresha umeme Sumbawanga hatua itakayoondoa mgao wa umeme. Trasfoma mpya yenye uwezo wa megawati 15 iliyojengwa katia kituo cha kupoza umeme Sumbawanga ambayo imekalimika hatua itakayoondoa tatizo la umeme mkoa wa Rukwa na sehemu ya Mkoa wa Katavi.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

Na. OMM Rukwa

Tanesco Mkoa wa Rukwa upo mbioni kukamilisha mradi wa kufunga transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 15 katika kituo cha kupozea umeme kilichopo Manispaa ya Sumbawanga hatua itakayomaliza tatizo la umeme wa mgao.

Hayo yamebainishwa jana (14 Machi,2022) na Meneja wa Tanesco mkoa wa Rukwa Mhandisi Fatael Maro wakati akitoa taarifa kwa wajumbe wa kamati ya Usalama ya mkoa huo iliyotembelea kituo cha kupoza umeme mjini Sumbawanga.

Mhandisi Maro alibainisha kuwa mradi huo unahusisha kujenga transfoma kubwa mpya na kujenga njia za umeme nne kwa wateja ambapo utawezesha kuongeza megawati 15 za umeme toka megawati 10 za sasa hivyo kuwa na uhakika wa umeme kwa mji wa Sumbawanga na wilaya za Nkasi ,Kalambo na wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

"Tuko katika hatua za mwisho za kufunga transfoma ambapo mkandarasi anajiandaa siku ya Jumapili ijayo (20 .03.2022) kuipa moto transfoma hiyo ili kufanya majaribio ya mwisho kabla kazi ya kuanza kupeleka umeme kwa wateja", alisema Mhandisi Maro

Akizungumza kwenye ziara hiyo fupi Mkuu wa Mkoa Rukwa Joseph Mkirikiti aliwataka wataalam hao wa Tanesco kumsimamia kwa karibu mkandarasi kampuni toka China ili kazi ikamilike mapema mwezi huu na wananchi wawe na uhakika wa umeme hatua itakayoondoa mgao uliopo sasa.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi wa kuboresha kituo cha umeme Sumbawanga Mhandisi Albert Msangi aliwajulisha wajumbe hao kuwa jumla ya shilingi Bilioni 3.8 zimetumika katika mradi huo unaohusisha ujenzi wa transfoma mpya yenye ukubwa wa MVA 15.

Mhandisi Msangi aliongeza kusema kituo hicho kitawezesha mkoa wa Rukwa kuwa na ziada ya umeme pia maeneo ya wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi yatapata umeme huo baada ya transfoma kubwa kukamilika hivi karibuni.

“Tukapowasha transfoma hii mpya itasaidia kumaliza tatizo la umeme wa mgao kwa mkoa wa Rukwa na wilaya ya Mlele kule Katavi” alisisitiza Mhandisi Msangi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala aliyeshiriki ziara hiyo alisema anaipongeza serikali kwa kufanikisha mradi huo muhimu kwa uchumi wa Rukwa na kuomba taarifa za kukamilika mradi huo ziwafikie viongozi wa chama mara kwa mara.

“Tumefurahi kuona mradi huu hapa Tanesco sasa tutausemea kwa wananchi ili wajue serikali inavyotatua changamoto ya upatikanaji nishati hiyo kwa mkoa wa Rukwa. Tunaohitaji Meneja wa Tanesco awe anatupatia pia taarifa za mradi huu, ili nasi tuwafikishie wana CCM" alisema Lukala.

Kwa sasa mkoa wa Rukwa unapokea umeme wake toka Jimbo la Mbala nchini Zambia

Post a Comment

0 Comments