****************************
Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuimarisha utafiti wa Kilimo nchini na kuwajengea uwezo watafiti wa kilimo waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi kwa kuongeza bajeti katika eneo hilo la utafiti ili kukuza sekta ya kilimo nchini.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa kilimo Mh. Anthony Mavunde wakati alipotembelea Taasisi ya utafiti wa kilimo nchini TARI katika makao makuu ya ofisi zake zilizopo Makutupora Jijini Dodoma na kuangalia kazi zinazofanywa na Taasisi hiyo.
“Mimi na Mh Waziri Bashe ni waumini wakubwa sana wa Sayansi.Kilimo ni sayansi,kilimo cha nchi yetu hakiwezi kuendelea pasipo kuwekeza kwenye utafiti na kuwajengea uwezo watafiti wetu.
TARI ninyi ni moyo wa kilimo nchini,msipofanya kazi nzuri sekta hii haiwezi kukua na hivyo nchi itashindwa kuyafikia malengo tuliyojiwekea ya kukuza uchumi,kuongeza nafasi za ajira na kupunguza umaskini wa watanzania.
Hii ndio sababu serikali inaona umuhimu wa kuimarisha utafiti wa kilimo nchini kwa kuongeza bajeti katika eneo hili ili kusaidia uzalishaji wa mbegu bora na ugunduzi wa mbegu bora sambamba na mafunzo zaidi kwa watafiti wetu lengo kuu likiwa ni kumsaidia mkulima wa Tanzania kuzalisha kwa tija”Alisema Mavunde
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya utafaiti wa kilimo nchini TARI Dkt Geofrey Mkamilo ameishukuru serikali kwa kulipa umuhimu eneo la utafiti ambapo katika bajeti ya mwaka 2020/21 walitengewa kiasi cha Tsh 7.3 bilioni na kwa bajeti ya mwaka 2021/22 imeongezeka kufikia Tsh 11.6 Bilioni,katika kipindi hiki Taasisi imefanikiwa, pamoja na mambo mengine,kugundua aina 5 za mbegu bora za mazao: Mbili (2) ni za ngano; moja(1) ya mpunga na mbili (2) za choroko.
0 Comments