












(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
*******************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali imezindua wa uvuvi wa meli ya Pacific Star ya wawekezaji wa kampuni ya Albacora ya nchini Uhispania pamoja na kuwakabidhi leseni ya uvuvi wa Bahari Kuu na kibari cha meli kuvua nje ya Mipaka ya Tanzania kwa maana ya meli kuwa imesajiliwa Tanzania.
Wawekezaji hao wanakwenda kuvua samaki katika bahari kuu, uwezo wa meli hiyo ambayo itatumika kuvua ni tani 2000 kwa mkupuo mmoja.
Hafla hiyo imefanyika leo Tarehe 21/03/2022 Jijini Dar eS Salaam mara baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki akiambatana na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame, Naibu Waziri wa Uvuvi Mhe.Abdalah Ulega pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kupokea meli hiyo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Waziri Ndaki amesema kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania inakuwa na meli kubwa ya uvuvi ambayo inapeperusha bendera yake na kuleta faida kubwa kwa watanzania.
Aidha amesema kupitia uwekezaji huo, Serikali itapata Dola Laki Nne kwa mwaka pamoja na samaki tani 300 ambao wanalengwa kuvuliwa vilevile na samaki wasiolengwa tani 100.
Pamoja na hayo amesema kutakuwa na mafunzo kwa mabaharia watano kwenye meli hiyo ambapo wawili kwa kila mwaka na kuweza kuongeza uwezo wetu wa kuvua kwenye maji marefu.
"Tuna muda mrefu sasa hatuna wataalamu wa uvuvi kwenye maji marefu, lakini hawa watatuanzishia ili tuweze kuwa na mabahari wazoefu katika uvuvi kwenye maji marefu". Amesema Mhe.Ndaki.
Hata hivyo amesema wawekezaji hao watajenga kiwanda cha kuchakata samaki, ambapo kwa muuda wa mwaka mmoja ujao tayari maendeleo hhayo yataanza kuonekana.
"Kukishajengwa kiwanda hapa, maana yake meli hii itakuja kushusha samaki hapa hapa badala ya kushusha kwenye nchi zingine na watanzania wengi watapata ajira pia wamesema kwa kuanzia wataweza kuajiri watanzania 100". Amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe.Suleiman Masoud Makame amesema ujio wa meli hiyo inajenga matumaini ya watanzania kwenye sekta ya uvuvi kwasababu katika makubaliano yao yamelenga kuifadisha Tanzania katika shughuli ambazo zitakuwa zinafanywa kwenye meli hiyo pia itakuwa ni meli kubwa ambayo itakuwa inapeperusha bendera ya Tanzania.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt.Christina Ishengoma amesema Jitihada za Serikali zimefanya tupokee meli ya wawekezaji ambapo itatuwezesha nasi tuweze kuvua samaki katika bahari kuu.
Dkt.Christina amepongeza juhudi za Serikali katika kuhakikisha wawekezaji wengi kuvutiwa na kuja kuwekezaji Tanzania ambapo ajira pia zinaongezeka.
0 Comments