Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI MHANDISI MASAUNI ATAJA MAFANIKIO YA WIZARA KATIKA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati akieleza mafanikio ya Wizara yake ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari wakati akieleza mafanikio ya Wizara yake ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita. Baadhi ya watumishi wa jeshi la Polisi wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Masauni akielezea mafanikio ya Wizara yake ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita.

*****************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni ameeleza maeneo ambayo Wizara yake inajivunia kufanya vizuri kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita Madarakani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 11, 2022 katika mkutano maalum Mhandisi Masauni amesema Wizara yake imefanya mambo mengi katika kuwatumikia Watanzania ambapo katika hayo ina maeneo yaliyofanikiwa zaidi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita katika Kipindi hiki cha Mwaka Mmoja, imetoa jumla ya Shilingi 14,591,092,573.99 ili kukamilisha Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa kwenye Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyoko chini ya Wizara hii ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Aidha amesema Wizara inaendelea na ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji Jijini Dodoma. Ujenzi huo unagharimu jumla ya Shilingi 20,283,091,685.

Ameeleza kuwa Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita, Vyombo vya Usalama vilivyoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vimeajiri jumla za askari 6,023.

"Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, jumla ya Maafisa, Wakaguzi, Askari na Watumishi raia 34,698 wamepandishwa vyeo, ambapo kati yao; 34,106 ni Maafisa, Wakaguzi na Askari na 592 ni Watumishi raia ambao walistahili kupandishwa vyeo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021". Amesema Mhandisi Masauni.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kusajili wananchi 1,061,998 katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, hivyo kufanya jumla ya Wananchi 22,881,902 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo.

"Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita zimetolewa Namba za Utambulisho 1,335,298 hivyo kufanya Mamlaka kuwa imetoa jumla ya Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) 19,283,241 tangu kuanza kwa zoezi hilo". Ameeleza.

Mhandisi Masauni amesema Wizara imefanikiwa kuokoa na kuwasaidia wahanga 102 wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu waliokuwa wakitumikishwa katika maeneo mbalimbali nchini. Wahanga wote wamepewa hifadhi na huduma muhimu katika nyumba salama.

Vilevile amesema Wizara kupitia Sekretarieti ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wadau 280 wanaohusika na utekelezaji wa Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu.

Post a Comment

0 Comments