Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape NNauye akizungumza na waandishi wa habari wakati akieleza mafanikio ya Wizara yake ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape NNauye akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati akieleza mafanikio ya Wizara yake ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita.
*****************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape NNauye ameeleza maeneo ambayo Wizara yake inajivunia kufanya vizuri kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita Madarakani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 11, 2022 katika mkutano maalum Waziri Nape amesema Wizara yake imefanya mambo mengi katika kuwatumikia Watanzania ambapo katika hayo ina maeneo yaliyofanikiwa zaidi.
Ameeleza kuwa Katika kipindi cha mwaka mmoja kumekuwa na ongezeko la account za simu kutoka account milioni 27.3 na kufikia account milioni 32.7 sawa na asilimia 19%.
Aidha amesema Wizara imefanikiwa kuondoa zuio la matangazo ya kubahatisha (online betting, Gambling) ambapo mwanzo yaliweza kuwekewa zuio.
"Matangazo na michezo ya kubahatisha inayofanyika katika mtandao yataendelea kusimamiwa na sheria ya nchi ya kubahatisha (gaming Act) hivyo Serikali iliona kwamba hakuna haja ya kuwa na zuio". Amesema Waziri Nape.
Amesema Wizara imefanikiwa kupunguza ada ya maombi ya leseni ya maudhui ya mtandaoni (online Media services for news and current affairs) kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 50,000 na ada ya mwaka toka shilingi 1,000,000 hadi 500,000.
Waziri Nape amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuondoa tozo katika vifaa vya TEHAMA, bunge lililopita la Bajeti tuliondoa kodi kwa vifaa kama laptop, Kompyuta na baadhi ya vifaa vya TEHAMA ili viweze kusambaa kwa wananchi wanaohitaji kutumia vifaa hivyo.
Vilevile amesema Katika Uongozi wa Rais Samia Suluhu,kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Februari 2022 laini zilizosajiliwa ni Milioni 55 ukilinganisha na laini Milioni 51.2 zilizosajiliwa awali sawa na ongezeko la asilimia 8%.
Hata hivyo amesema imetenga shilingi Bilioni 170 kuwezesha kujengwa kwa mkongo wa Taifa ambapo Wizara imeingia mkataba wa mashirikiano na shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwaajili ya kufanya kazi pamoja ya kupitisha miundombinu ya mawasiliano kwenye miundombinu ya umeme kwa lengo la kuongeza mtandao wa mawasiliano wa umeme.
"Serikali imekamilisha ukarabati wa Kilomita 105 za ujenzi wa mkongo kati ya jiji la Arusha na Namanga kupitia kwenye miundombinu ya TANESCO". Amesema
0 Comments