************************
NA WAF. DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya imesaini mpango wa utekelezaji wa afua za afya za kila mwaka unaoandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambao unazingatia vipaumbele vya Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya (2021/22-2025/26).
Mpango kazi huo wenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 21.48 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 49.6 umesainiwa mapema leo Machi 08, 2022 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa WHO nchini Dkt. Tigest Ketsela katika Ofisi za Wizara, jijini Dodoma.
Mpango huo unalenga maeneo makuu sita ambayo ni: Kufikisha Afya kwa wote, Huduma za Dharura na kukabiliana na majanga, Afya na Ustawi, Uwezeshaji katika Mifumo ya Afya, Kukabiliana na kudhibiti magonjwa ya mlipuko na kutekeleza miradi ya kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Akiongea wakati kusaini mpango kazi huo, Waziri Ummy ameishukuru WHO kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini ambapo amesema Serikali ya awamu ya sita inaendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi lakini peke yake haitaweza bila kushirikiana na wadau.
Kwa upande wake Dkt. Tigest amemwambia Waziri Ummy kuwa WHO iko tayari muda wote kusaidiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha uboreshaji wa huduma za afya zenye kuzingatia usawa na kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa.
0 Comments