Ticker

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA ARDHI YASHIRIKIANA NA KOREA KUBADILISHA MIFUMO YAKE KUWA YA KIDIGITALI


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mtendaji Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions Co Ltd ya Korea Kusini baada yeye na ujumbe wake kumtembelea ofisini kwake eneo la Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe 30 Machi 2022.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akimvisha vazi la kimasai Mtendaji Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions Co Ltd ya Korea Kusini baada ya kumtembelea ofisin ya Wizara ya Ardhi eneo la Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe 30 Machi 2022.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Korea Kusini ulioongozwa na Mtendaji Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions Co Ltd Munseok Lee mara baada ya kumtembelea ofisini kwake eneo la Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe 30 Machi 2022.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na ujumbe kutoka Korea Kusini ulioongozwa na Mtendaji Mkuu na Rais wa Kampuni ya Hojung Solutions Co Ltd Munseok Lee baada ya kumtembelea ofisini kwake eneo la Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma tarehe 30 Machi 2022.

***********************

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ushirikiano wake na Korea Kusini imeanzisha mkakati wa kuhakikisha inabadilisha mifumo yake upangaji, utumiaji, upimaji na uwekaji kumbukumbu za sekta ya ardhi kutoka analogia kwenda digitali ili kuboresha sekta ya ardhi.

Hatua hiyo inafuatia mifumo mingi ya upangaji, utumiaji upimaji na uwekaji kumbukumbu za ardhi katika Wizara ya Ardhi kuendelea kutumia mifumo ya analogia katika upangaji, utumiaji, upimaji na uwekaji kumbukumbu za sekta ya ardhi.

Katika kufanikisha azma hiyo Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Serikali ya Korea Kusini zimeingia makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji mradi wa ujenzi wa kituo cha Kisasa cha Mafunzo pamoja na uboreshaji miundombinu ya sekta ya ardhi.

Hayo yamebainishwa tarehe 30 Machi 2022 jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi wakati akielezea ushirikiano baina ya serikali ya korea kusini na Wizara ya ardhi katika uanzishaji kituo cha kisasa cha kutolea mafunzo kwa wataalamu wa upimaji pamoja na uboreshaji miundombinu ya sekta ya ardhi.

Uanzishwaji Kituo cha kisasa utagharimu fedha za kitanzania Shilingi Bilioni 5.2 na ule wa ujenzi wa miundombinu utagharimu dola milioni 64.

Akielezea ujenzi wa kituo cha kisasa, Dkt Kijazi alisema uanzishwaji wa kituo hicho siyo tu kwa ajili ya kutumia teknolojia ya kisasa pekee bali ile itakayoendana na wakati ambapo kupitia mradi huo Wizara ya Ardhi itapokea msaada wa kiufundi sambamba na wataalamu wake kupatiwa mafunzo na kuwekewa vifaa vinavyohusu mifumo ya ardhi.

‘’Pamoja na kuwekwa vifaa kwenye kituo lakini pia watumishi watajengewa uwezo pamoja na kukusanya, kuchakata na kutumia takwimu za ardhi katika mipango ya kuendeleza sekta ya ardhi’’ alisema Dkt Kijazi.

Akigeukia sehemu ya pili ya mradi huo, Dkt Kijazi alisema, itakuwa ni ujenzi wa miundombinu itakayowezesha wizara ya Ardhi kutumia teknnolojia ya kisasa katika masuala mazima ya kupanga, kupima na kutumia takwimu za ardhi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi..

Mradi mzima utahusisha uandaaji ramani za uwiano mdogo na zile za uwiano mkubwa kwa ile miji mikuu ya mikoa 26 ya Tanzania Bara sambamba na kuweka vituo vya kielektroniki vya upimaji ardhi na kuboresha miundombinu ya kusambaza taarifa za kijografia kwa idara za serikali na watumiaji wote nchini.

Katika hatua nyingine, ujumbe wa wataalamu kutoka Korea kusini uliokuja kwa ajili ya hatua za awali za utekelezaji miradi hiyo ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Hojung Solution Co Ltd Munseok Lee umekutana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwa ajili ya kujitambulisha na kumuelezea maendeleo ya utekelezaji miradi hiyo.

Ujumbe huo ulimueleza Dkt Mabula uko tayari kuanza kazi ya utekelezaji mradi huo baada ya maandalizi ya awali ya kutoa mafunzo kwa baadhi ya watumishi nchini.

Kwa upande wake Dkt Mabula aliuambia ujumbe huo kuwa ana imani ujumbe huo ulishiriki vyema hatua zake za awali za maandalizi ya utekelezaji mradi huo na kueleza kuwa matarajio yake kila kitu kitaenda vizuri katika utekelezaji mradi huo.

Post a Comment

0 Comments