Ticker

6/recent/ticker-posts

AJALI YAUA 6 YAJERUHI 19 KOROGWE MKOANI TANGA**************

Na Hamida Kamchalla, Korogwe.

WATU 6 wamefariki dunia na wengine 19 kujeruhiwa baada ya gari aina ya Costa, yenye namba T 833 DMH, kugonga nguzo ya daraja na kutumbukia baada ya dereva wa gari hilo kushindwa kulidhibiti kutokana na mwendo wa kasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Safia Jongo alithibitisha na kusema ajali hiyo imetokea saa 9 alfajiri kuamkia jumanne tarehe 12 ambapo gari hiyo ilikuwa ikitokea Dar es salaam kuelekea mkoani Kilimanjaro kupeleka msiba.

Jongo alibainisha kwamba ajali hiyo ambayo imehusisha Wanawake watatu na wanaume watatu imetokea katika eneo la Kwamduru, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, ambapo kati ya wanawake hao mmoja alikuwa ni mtoto mdogo mwenye umri kati ya miaka miwili na minne na miili mitano imeshatambuliwa na ndugu zao lakini mmoja bado hajatambuliwa wakati hali za majeruhi zinaendelea vizuri na wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Magunga.

"Kwa kifupi tu ni kwamba, ile Costa ni zile zinazokodishwa kwahiyo ina vibali, inavyoonekana alitengeneza mazingira Kama wamekodiwa, walipopita sehemu mbili Askari waliwakagua, walikuwa na vibali vyote na walikuwa wanaelekea msibani Kilimanjaro" alisema Kamanda.

"Kwasababu wakitoka huko huwa wanakubaliana waseme wamekodiwa, lakini baada ya ajali hii kutokea na kufanya mahojiano ya kina na abiria, walisema kwamba pale Ubungo walikatiwa tiketi na kuingia kwenye gari kama abiria" alibainisha.

"Natoa wito kwa wananchi, kutokana na ajali hii tujifunze, vitu vyote ambavyo huwa havifuati taratibu, basi mwisho wake siyo mzuri, safari za usiku ambazo siyo rasmi matokeo yake yanakuwa kama haya" aliongeza Jongo.

Aidha Kamanda Jongo alisema dereva wa gari hilo ni miongoni mwa majeruhi na amelazwa hospitali hapo akipatiwa matibabu chini ya ulinzi wa jeshi la polisi, na kuongeza kuwa mara kwa mara wanatoa maelekezo kwa madereva kuwa makini kwa kutoendesha mwendo wa kasi lakini pia kuheshimu na kufuata sheria na alama za barabarani.

"Kwahiyo niendelee kuwasihi madereva wafuate sheria na alama za barabarani wasisubiri mpaka wakutane na Askari, hii itatusaidia kupunguza hivi vifo, lakini kila mwananchi awe ni balozi wa usalama barabarani, pale anapoona dereva anaendesha mwendo hatarishi atoe taarifa kwasababu majeruhi hawa wanakiri kwamba pale ambapo dereva wao alipokaribia kuwafikia polisi alikuwa akiendesha mwendo wa taratibu" alisema.

Naye Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Korogwe Dr. Salma Swed akiongea kwa njia ya simu baada ya kuhakikisha taarifa hiyo kutoka kwa mganga aliyemkaimu, alikiri kupokea miili ya marehemu na majeruhi alfajiri ya kuamkia siku ya jumanne na kusema, "tumepokea miili ya marehemu 6 na majeruhi 19 lakini wawili kati yao Hali zao ni mbaya na tumewahamishia katika hospitali ya rufaa ya Bombo".

Post a Comment

0 Comments