Ticker

6/recent/ticker-posts

MADEREVA WA BODABODA NA CHANGAMOTO YA UVAAJI WA HELMET




****************************


Na Hamida Kamchalla, Tanga.


Madereva wa bodaboda wilayani Tanga wametoa malalamiko yao kwamba wamekuwa wakipata changamoto na abiria wao ambao hawataki kuvaa kofia ngumu (helmet) kutokana na sababu za kuwepo kwa magonjwa ya ngozi kwakuwa zinavaliwa na mtu zaidi ya mmoja.


Aidha walisema sababu hiyo imepelekea hata wakiwa na abiria bila kofia hiyo hata Askari wa barabarani hawachukui hatua na watu wengi wamejiaminisha kwamba sababu hiyo imekubalika, lakini pia walisema wao hawana uwezo wa kununua kofia zaidi kutokana na hali ngumu ya kipato.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya madereva walisema kwa sasa hawana hofu ya kukamatwa na Askari juu ya kofia hizo kutokana na kuwepo kwa ukweli wa abiria wao huku hoja ya maambukizi ya magonjwa ya ngozi ina asilimia kubwa kuchangiwa na zoezi hilo.


"Hali ya siku hizi ni ngumu sana, na sababu tulizonazo zote zinakwenda kugonga kwenye ukweli, kwanza kwetu sisi madereva kipato chetu ni kidogo mno, hapa tunahangaika tu ilimradi tusikose kazi za kufanya, kwa maana nyingine namaanisha tunakwepa kukaa vijiqeni" alisema Mussa Haji, dereva kituo cha sabasaba.


"Uwezo wa kununua kofia mbili tunavyojijua hatuna, yaani mbali na abiria wetu kuzikataa kwa madai ya maambukizi ya magonjwa ya ngozi na sababu hii pia ukiangalia ina ukweli ndani yake, maana utakuta abiria mwengine ni daktari na anakwambai kabisa sivai ukikamatwa mimi nitajibu, hapo unajikuta huna nguvu ya kubishana tena, alisisitiza Haji.


Aidha walibainisha kwamba kwasasa zoezi hilo ni kama limekufa maana hata wakisimamishwa barabarani hawaulizwi kuhusu kofia ya pili ambayo ilitakiwa kutembea nayo wakati wote maalumu kwa ajili ya kuvaliwa na abiria utakayempakia.


Lakini pia waliuomba uongozi wa Mkoa kuliangalia upya suala hilo na kuacha lipite badala ya kulifikiria kulifufua kutonaka na sababu zilizotolewa ili vijana wengi wanaofanya biashara ya bodaboda wasiweze kurudi tena mitaanu na kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa.


"Ujue vijana wengi wanaoendesha bodaboda kwasasa wametokea vijiwe, na ndiomaana ukaona wengi wetu hapa tunapiga deiwaka tu, leo tajiri katulia anakukabidhi chombo jioni anataka mahesabu, na kuna wengine mnaingia mikataba, hapa sasa wapo wanaofanikiwa kumaliza mkataba wao wanachukua chombo lakini wengine hawamalizi, tajiri anachukua chombo yake na pesa uliyotoa hupati" alisema Faraji Kitundu, dereva kituo cha barabara 12.


Baadhi ya abiria nao walisema ni vema kitengo cha usalama barabarani kutafuta njia mmbadala ya kufanya ili kuweza kudhibiti usalama wa bodaboda na abiria wao kuliko kutumia hizo kofia kutokana na hali ya usalama wa kiafya, kwani utavaa kofia utajikinga barabarani ukitoka hapo unavua anavaa mwengine bila kujali aliyetoka kuvaa ana tatizo gani.


"Hii siyo sawa kabisa, binafsi yangu aiwezi kuvaa, kuna magonjwa ya ngozi kila sehemu ya mwili wa binadamu, yaani chamsingi hapa ni wao Askari kutafuta mbinu nyingine itakayoweza kusaidia ili kuepukana na haya makofia lakini pia kutuepushia maradhi ambayo ukiyapata unaona kabisa ni ya makusudi" alisema Farhiya Swalehe, mkazi wa Mabawa.


Akizungumzia jambo hilo Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga Leopard Fungu alisema suala la kuvaa kofia ngumu kwa dereva na abiria wake lilipitishwa na bunge kisheria hivyo ni lazima Sheria hiyo isimamiwe vema ili kuepusha madhara yanayojitokeza ya ajali za barabarani.


"Ajali ya pikipiki ikitokea, kiungo cha kwanza kizito katika mwili wa binadamu ni kichwa, hivyo basi mtu yeyote ambaye hajavaa helmet inapotokea anapata ajali madhara yake ni makubwa, aidha majeraha makubwa au kifo, na Kama atakuwa na majeraha makubwa basi atapata utindio wa ubongo ambao unaweza kumpelekea kuchanganyikiwa" alisema.


Aidha Fungu alibainisha kwamba watengenezaji wa pikipiki walijua madhara ya kutokuvaa helmet na ndiyo maana wakatengeneza ili mtu akinunua pikipiki anapata na helmet hizo mbili kwa ajili ya dereva na abiria wake.


"Suala la kusema ukatae kuvaa helmet kwasababu ni chafu unaogopa magonjwa ya ngozi, siyo kweli, unaporidhia kwenda kupanda bodaboda basi jihakikishie unajiandaa, kuna vikofia vyepesi au hata unatanguliza nguo itakayokukinga na kuweza kuvaa helmet" alibainisha.


"Nitoe wito kwamba, kila mwenye bodaboda lazima awe na kofia mbili iwa ajili yake na abiria wake, tusidharau mambo haya ya kisheria, wale wanaozitunga wanajua ninkwasababu ya ulinzi na usalama pale tunapopata ajali" alisisitiza Fungu.


Hata hivyo alisema misako ya kuwakamata wasiovaa helmet inaendelea na watu wanakamatwa na wengine wakiwa na makosa zaidi ya kuvaa hizo kofia, na kwamba ameshangazwa na baadhi ya madereva kuendesha vyombo hivyo vya moto bila kuwa na kioo kinachomuonesha kunachokuja nyuma yake.


"Lakini nashangaa kwanini Tanga baadhi ya watu wanakuwa siyo waelewa sana, lakini nilichokuja kukiona mpaka side mirror wanazitoa wakati lile ni jicho la tatu, ni vitu vya kushangaza sana, sijui ni mwalimu kipofu nani ambaye amewaambia kitu kama hicho, na hatutasita kuwakamata wote" aliongeza.

Post a Comment

0 Comments