Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. NDALICHAKO AZINDUA MPANGO WA TATHMINI YA USALAMA, AFYA- OFISI ZA WIZARA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa ukaguzi,mafunzo na upimaji afya kwa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliofanyika katika jengo la OSHA, Jijini Dodoma, Aprili 20, 2022.


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (wa pili kutoka kushoto) akieleza namna Taasisi hiyo imejipanga kutekeleza mpango wa ukaguzi,mafunzo na upimaji afya kwa Wafanyakazi wa Wizara mbalimbali wakati wa uzinduzi wa mpango huo. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako. Wa pili Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu (wa pili kutoka kushoto) akieleza jambo wakati wa hafla hiyo.


Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya OSHA, Dkt. Adelhelm Meru akitoa neno la shukrani mara baada ya hafla ya uzinduzi wa mpango wa ukaguzi,mafunzo na upimaji afya kwa Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliofanyika katika jengo la OSHA, Jijini Dodoma, Aprili 20, 2022.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akipima macho kwa kutumia mashine ya kisasa ikiwa ni sehemu ya uzinduzi rasmi wa upimaji wa afya kwa watumishi wa Wizara mbalimbali wakati wa hafla hiyo.


Sehemu ya watumishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Wakala wa Usalama Mahala pa Kazi (OSHA) wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa ukaguzi, mafunzo na upimaji afya kwa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu uliofanyika katika jengo la OSHA, Jijini Dodoma, Aprili 20, 2022.

*****************************

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amezindua mpango maalum wa kutathmini mazingira ya kazi katika ofisi zote za serikali utakaofanyika sambamba na upimaji wa afya za wafanyakazi wote pamoja na kuwapa mafunzo stahiki ya usalama na afya mahali pa kazi.

Prof. Ndalichako amesema mpango huo utatekelezwa kwa mwezi mmoja kuanzia Aprili 20, 2022 ambapo utahusisha mambo mbali mbali ikiwemo; Ukaguzi wa Mifumo ya Usalama katika Ofisi za Wizara mbali mbali ikiwemo miradi ya ujenzi katika Mji wa Serikali-Mtumba.

Mambo mengine ni pamoja; Uchunguzi wa afya za wafanyakazi, Mafunzo ya Huduma ya Kwanza mahali pa kazi pamoja na mafunzo kwa Wawakilishi wa Kamati za Usalama na Afya mahali pa kazi yatakayoambatana na uundaji wa Kamati husika.

”Kimsingi OSHA ina wajibu wa kulinda nguvukazi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake. Kwa mujibu wa Sheria tajwa, OSHA inapaswa kuhakikisha kwamba inayatambua maeneo yote ya kazi nchini kwa kuyapatia usajili na kisha kuyafikia kwa ajili ya kufanya tathmini ya hali ya mazingira ya kazi, kutoa mafunzo stahiki kwa wafanyakazi pamoja na kuchunguza afya za wafanyakazi kutegemeana na shughuli wanazozifanya,” amesema Prof. Ndalichako.

Akizungumza mara baada ya mpango huo kuzinduliwa, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema mpango huo ni mwendelezo wa mkakati wa Taasisi yake wa kufanya tathmini ya mazingira ya kazi nchini kisekta.

“Leo tumezindua mpango huu wa ukaguzi, mafunzo na upimaji afya kwa wafanyakazi wote wa serikali tukianza na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo programu hii ni mwendelezo wa makakati wetu wa kuzifikia sekta zote za uchumi kikamilifu. Lengo la zoezi hili ni kuandaa rejista ya vihatarishi vya kila sekta na hivyo kurahisisha uaandaji wa mikakati ya kukabiliana na vihatarishi hivyo katika kila sekta,” amesema Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA.

Baadhi ya wafanyakazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu waliohudhuria hafla ya uzinduzi, wametoa maoni yao kuhusu mpango huo ambapo wamesema utasaidia katika kuboresha mazingira yao ya kazi.

“Kwaujumla mpango huu ni mzuri sana na utatusaidia watumishi kufanya kazi zetu kwa kuzingatia tahadhari muhimu dhidi ya vihatarishi mbali mbali. Aidha, kupitia mpango huu ambao utahusisha tathmini ya kina ya mazingira ya kazi, itakuwa ni fursa muhimu kwa mwajiri wetu kuboresha mazingira ya kazi kutokana na mapendekezo yatakayotolewa na wataalam wa OSHA,” amesema Aloyce Kirumbi ambaye ni Afisa Utumishi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri Prof. Ndalichako katika uzinduzi, mpango huo utatekelezwa kwa mwezi mmoja ambapo mazingira ya kazi katika Wizara zote yatafanyiwa ukaguzi na wataalam wa OSHA. Aidha, baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, yatatolewa mapendekezo ya kitaalam ambayo yatatumika na serikali katika kuboresha mazingira ya kazi.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye jukumu ya kulinda nguvukazi ya nchi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo hufanya utambuzi wa maeneo ya kazi na kuyafikia kwa ajili ya ukaguzi, mafunzo ya usalama na afya pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi.

Post a Comment

0 Comments