Ticker

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA AFYA NA WHO KUSHIRIKIANA KATIKA KUTOKOMEZA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA NA YASIYO YA KUAMBUKIZA NCHINI.


*****************************

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na shirika la afya duniani (WHO) imezindua mpango mkakati wa kutekeleza afua mbalimbali za afya ikiwemo udhibiti wa magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.

Mpango huo utakaogharimu Tsh. Bilioni 145 katika kipindi cha miaka mitano (2022-2027) umezinduliwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu jijini Dar Es Salaam.

Waziri Ummy amesema kupitia mpango uliopita nchi imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano kwa kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza kama malaria, kifua kikuu na UKIMWI pamoja na vifo vya mama na mtoto na kwamba changamoto zilizopatikana zimewekwa ndani ya mpango mkakati mpya.

"Tumezindua mpango kazi wa miaka mitano ya ushirikiano kati ya WHO na Serikali ya Tanzania bara pamoja na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, tukitarajia kupata msaada wa kiufundi katika maeneo mbalimbali kutoka WHO ikiwa ni kutekeleza mikakati mbalimbali ya afya ikiwemo kupambana na haya magonjwa yanayotolewa taarifa na WHO kama ilivyo kwa Uviko-19". Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ameongeza kuwa magonjwa kama Ebola, Kipindupindu ni maeneo ambayo yamebainishwa katika mpango huo yatafanyiwa kazi kwa ukaribu, na kuongeza kuwa eneo la pili ni afya ya mama na mtoto ambapo wataendelea kushirikiana katika kutatua changamoto.

Waziri Ummy pia ametaja eneo la ubora wa huduma akisema licha ya kujengwa kwa zahanati lakini majengo pekee hayatoshi, huduma na rasilimali watu vinahitajika na kwamba Rais Samia ametoa ajira zaidi ya 12,000 za afya ili kutatua changamoto hiyo.

Kwa upande wake Mwakilishi mkazi wa WHO nchini Mengetsu Ketsela amesema WHO itaisaidia Tanzania katika maeneo sita ikiwemo hali ya afya na usawa, usawa wa kijinsia na haki za binadamu, dharura za afya, mfumo wa taarifa za afya, ushirikiano na kuweka vipaumbele vya kimkakati.

Nae Waziri wa afya wa Zanzibar Dkt. Ahmed Mazrui amesema ushirikiano huo utasaidia kutatua changamoto za afya katika maeneo mbalimbali na ni mpango ambao Tanzania imeuridhia na utaendelea kutekelezwa.

Post a Comment

0 Comments