Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MULAMULA AMWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA DHARURA AU

Na Mwandishi wetu, Malabo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea tarehe 27 na 28 Mei, 2022.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine, umejadili ajenda kuu mbili ambazo ni majanga na huduma za kibinadamu, masuala ya Ugaidi na Mabadiliko ya Serikali yasiyozingatia misingi ya Katiba.

Akiongea wakati wa Mkutano huo, Balozi Mulamula amesema anamwakilisha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo ulioitishwa na na Umoja wa Afrika (AU) kwa lengo la kuangalia na kujadili maajanga na huduma za kibinadamu pamoja na ugaidi.

“AU wameitisha mkutano huu kwa lengo la kujadili namna ya kukabiliana na majanga haya na jinsi gani Bara la Afrika linaweza kuwa na mkakati wa pamoja wa kukabiliana na majanga haya, na tunategemea baada ya kikao cha leo tutapata azimio la kukabidiliana na majanga haya katika bara letu la Afrika,” amesema Balozi Mulamula.

Kuhusu masuala ya Ugaidi, Balozi Mulamula ameongeza kuwa, Mkutano wa kesho tarehe 28 Mei, 2022 mkutano utaendelea kuangalia masuala ya kigaidi na kuona ni jinsi gani Bara la Afrika linasimama kwa umoja wake kupambana na majanga ya kigaidi.

Awali akifungua Mkutano huo, Rais wa Senegali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mhe. Macky Sall amezisihi nchi za Afrika kuwa na umoja ambao utaziwezesha kukabiliana na majanga ya kibinadamu na mapambano dhidi ya ugaidi kwa urahisi zaidi.

Mhe. Sall amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano na mshikamano na kujenga uwezo wa kila nchi ili kuweza kukabiliana na majanga mbalimbali ya asili na wakati huo huo, kushughulikia changamoto za ulinzi na usalama ili kutozalisha wakimbizi na wahamaji ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano na kuunda Jeshi la Afrika (ASF) na Brigedi za kikanda pamoja na kuanzisha Vikosi Maalum kushughulikia Changamoto za Ugaidi.

Balozi Mulamula katika mkutano huo, ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe. Innocent Shiyo ambaye anawakilisha pia Umoja wa Afrika, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja na watumishi wengine waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa tayari kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea tarehe 27 na 28 Mei, 2022
Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Abiy Ahmed Ali akiteta jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula walipokutana katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Bw. Moussa Faki Mahamat akihutubia katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea
Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Macky Sall akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mkutano huo leo Jijini Malabo, Equatorial Guninea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na baadhi ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea
Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
Sehemu ya Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo, ambaye pia anawakilisha Umoja wa Afrika, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz pamoja na watumishi wengine waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mkutano ukiendelea
Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano wa Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea
Sehemu ya Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano wa Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika Malabo, Equatorial Guinea


Post a Comment

0 Comments