Ticker

6/recent/ticker-posts

RC MBONI: SHINYANGA TUPO TAYARI KUFANIKISHA UWEKEZAJI

 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amepongeza juhudi za Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) katika utekelezaji wa mikakati ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, kufuatia ziara ya kikazi ya mamlaka hiyo mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Uwekezaji wa Ndani inayoendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika Januari 29,2026, Mhe. Mboni alisema kuwa uwepo wa miundombinu bora ni kichocheo muhimu katika kuvutia na kulinda uwekezaji endelevu, akibainisha kuwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji wanapata huduma stahiki na mazingira rafiki kwa maendeleo ya biashara na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Mhe. Mboni alisisitiza kuwa Mkoa wa Shinyanga umejipanga kimkakati kupokea uwekezaji mkubwa zaidi, kupitia maeneo maalum yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya uwekezaji, sambamba na kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani ili Watanzania wajitokeze kwa wingi kuwekeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi ndani ya mkoa huo.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Mkoa itaendelea kushirikiana kwa caribou na TISEZA pamoja na wadau wengine wa uwekezaji, kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa miradi, kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza, na kuhakikisha kuwa Shinyanga inanufaika kikamilifu na fursa za uwekezaji zilizopo.

Kwa upande wake, TISEZA iliipongeza Uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano na utayari wake wa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji, huku ikisisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kuwafikia wawekezaji wa ndani, kutoa elimu ya uwekezaji, na kuchochea ushiriki mpana wa Watanzania katika maendeleo ya uchumi wa taifa.


Post a Comment

0 Comments