Ticker

6/recent/ticker-posts

JAJI MDEMU AWATAKA WATUMISHI IJC DODOMA KUBADILI FIKRA NA MITAZAMO KATIKA UTENDAJI

Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu amewataka watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) jijini Dodoma kuwa tayari kupokea mabadiliko ya kifikra na mitazamo katika utendaji kazi, na wala wasikubali kuishi na kufanya kazi kwa mazoea.

Akifungua mafunzo ya siku tano kwa watumishi wa kituo Jumuishi cha utoaji haki mapema jana tarehe 30, Mei 2022 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma, Jaji Mdemu alisema, sehemu ya mafunzo haya yanalenga kubadili mitazamo ya watumishi ambayo kwa hakika pamoja na kuondoa dhana ya kufanya kazi kwa mazoea, lakini pia mabadiliko ya kifikra na mitazamo yataongeza tija na ufanisi na pia kuwafanya watumishi wa Mahakama wafanye kazi kisasa zaidi.

“Naamini kubadili mtazamo kunaendana na maadili pamoja na tamaduni za kimahakama tulizonazo ndizo zinazotoa tafsiri ya namna umma tunaotumikia kutupima na hivyo kutoa taswira halisi ya utumishi wetu na pia Mahakama kama mhimili”, alisema Jaji Mdemu

Jaji Mdemu aliongeza kuwa, suala la maadili ni la lazima na ni wajibu wa kila mmoja kuyazingatia. "Si suala la hiari. Akawakumbusha washiriki kuwasikiliza watoa mada kwa utulivu wa hali ya juu na kufuatilia kwa makini mafunzo hayo kwani baadhi ya mada zinalenga masuala ya maadili."

Mabadiliko ya kifikra na mitazamo yaendane na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni jambo la kimkakati katika utoaji wa huduma za kimahakama. Uwekezaji uliofanyika katika usimikaji wa mifumo ya matumizi ya TEHAMA ni mkubwa na umetumia fedha nyingi.

Jaji Mdemu alitoa wito kwa washiriki wa mafunzo kujielekeza katika kuitumia mifumo hiyo ipasavyo kwani manufaa ya kuitumia ni makubwa zaidi hasa katika kuwahudumia wananchi kwa kuokoa muda, uwazi, ufanisi na uwajibikaji.

“Natambua kuwa mafunzo haya yamehusisha watumishi wa kada zote waliopo katika kituo hiki cha utoaji haki. Naomba nitumie hadhira hii kuwakumbusha mambo machache. Kwanza kabisa ni kuhusu uboreshaji wa huduma za Mahakama unaoendelea. Katika eneo hili, Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika ujenzi wa miundombinu ya majengo ikiwemo hili mnalolitumia, hii ni ushahidi tosha wa haya ninayoyaongea”, aliongeza Jaji Mdemu.

Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 ambapo katika Tunu ya Tano kuhusu weledi, Mahakama itatekeleza majukumu ya utoaji haki kwa umahiri na ufanisi.

Nguzo ya kwanza ya Mpango Mkakati wa Mahakama inayohusu Utawala Bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa rasilimali, Mahakama ya Tanzania inanuwia kuwa na uamuzi bora ambapo pia imejiwekea malengo ya kukuza uelewa wa misingi ya taaluma ya kisheria na kuongeza ujuzi kwa watumishi wa Mahakama. Katika kutekeleza malengo haya, Mahakama ya Tanzania imeweka Mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama wa ngazi zote.

Aidha, mada zitazofundishwa kwenye mafunzo hayo ni kama vile Tunu na utamaduni wa Mahakama ya Tanzania (the Judiciary of Tanzania Core values and culture), Mkataba wa Huduma kwa mteja (the Client Service culture), Kuweka uwiano wa taaluma na wajihi (balancing professionalism and personality), masuala ya saikolojia (psychological issues), masuala ya maadili (Code of Good conduct), utamaduni kwa muktadha wa mahakama (customized ethics in the judiciary of Tanzania), namna ya kuhudumia wateja kwenye vituo jumuishi vya utoaji haki(customer care and service delivery of standards of IJCs) na utoaji wa huduma ya kwanza (provisional of first aid).




Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu (aliyesimama) akizungumza na Washiriki wa Mafunzo ambao ni Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma tarehe 30 Mei, 2022.Amewataka watumishi wa Kituo hicho kuwa tayari kupokea mabadiliko ya kifikra na mitazamo katika utendaji kazi, na wasikubali kuishi na kufanya kazi kwa mazoea. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi na kulia ni Afisa Utumishi kutoka kitengo cha Mafunzo Mahakama ya Tanzania, Bw. Rajab Singana.




Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) jijini Dodoma wakifuatilia mada inayofundishwa na mtoa mada kuhusu utoaji wa huduma ya kwanza, Mafunzo hayo yanaendelea katika ukumbi wa mikutano wa Kituo wa Kituo hicho.
Sehemu ya Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) jijini Dodoma wakifuatilia mada inayotolewa na Mwezeshaji katika mafunzo hayo.
Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia mada inayofundishwa.
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma (wa kwanza hadi wa nne walioketi upande wa kushoto) wakiwa na Watumishi wengine wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) jijini Dodoma wakifuatilia mada inayotolewa katika mafunzo hayo.

Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu wanaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Jijini Dododma ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Gerson Mdemu (katikati), wa pili Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi, wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Aloyce Katemana na wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi Mahakama ya Tanzania, Bw. Rajab Singana
Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi kada ya Wasaidizi wa Kumbukumbu wanaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Jijini Dodoma ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu (katikati), wa pili Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi, wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu- Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Aloyce Katemana na wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi Mahakama ya Tanzania, Bw. Rajab Singana
Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa kada ya Wasaidizi wa Ofisi wanaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Jijini Dodoma ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Gerson Mdemu (katikati), wa pili Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi, wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu- Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Aloyce Katemana na wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi Mahakama ya Tanzania, Bw. Rajab Singana

Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi kada ya madereva wanaohudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Jijini Dodoma ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Gerson Mdemu (katikati), wa pili Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi, wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi, wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Aloyce Katemana na wa kwanza kulia ni Afisa Utumishi Mahakama ya Tanzania, Bw. Rajab Singana


(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

Post a Comment

0 Comments