Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA SWEDEN


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mheshimiwa Ann Linde, mazungumzo yaliofanyika mjini Stockholm leo tarehe 3 Juni 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akimkabidhi zawadi Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mheshimiwa Ann Linde, mara baada ya mazungumzo yaliofanyika mjini Stockholm leo tarehe 3 Juni 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mheshimiwa Ann Linde, mara baada ya mazungumzo yao yaliofanyika mjini Stockholm leo tarehe 3 Juni 2022.

*************************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 3 Juni 2022 amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Mheshimiwa Ann Linde, mazungumzo yaliofanyika mjini Stockholm nchini Sweden.

Makamu wa Rais amesema Tanzania na Sweden zimekua na ushirikiano mzuri wa muda mrefu na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kuimarisha uhusiano uliopo baina ya mataifa hayo mawili. Aidha ameishukuru serikali ya Sweden kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Elimu, Biashara pamoja na Haki za Binadamu.

Makamu wa Rais amesema nchi ya Sweden imepiga hatua katika sekta ya Afya hasa kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo na kusema ipo haja ya mataifa hayo kushirikiana katika kutoa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania. Ameongeza kwamba mataifa hayo mawili yanaweza kurejesha ushirikiano uliokuwepo hapo awali katika sekta ya Elimu ya juu uliochochea upatikanaji wa wataalamu mbalimbali nchini Tanzania.

Pia Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuimarisha sekta ya viwanda, uhifadhi wa mazingira, kuimarisha sekta ya kilimo pamoja na kuwekeza katika huduma za kijamii kama vile Elimu na Afya.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Ann Linde ameipongeza serikali ya Tanzania kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua ikiwemo kuimarika kwa haki za binadamu, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na demokrasia. Aidha amesema serikali ya Tanzania imefanya jambo la muhimu kutoa haki kwa wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo kwa kutambua elimu ndio nguzo muhimu kwa maisha yao.

Waziri Linde amesema upo uwezekano wa Tanzania na Sweden kuongeza zaidi ushirikiano hasa wa kibiashara kwa manufaa ya mataifa yote mawili kutokana na uwepo wa miundombinu kama reli na mabasi yaendayo haraka nchini Tanzania.



Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo nchini Sweden kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 wenye lengo la kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususani katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na janga la Uviko 19.

Post a Comment

0 Comments