Ticker

6/recent/ticker-posts

TUTAENDELEA KUHESHIMU MCHANGO WA MADHEHEBU YA DINI-MAJALIWA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Wolfgang John Pisa katika Ibada ya kumsimika Askofu huyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni 26, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Ibada ya kumsimika Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Wolfgang John Peter kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni 26, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu wa Kanisa Katoliki wakati aliposhiriki katika Ibada ya kumsimika Askofu Wolfgang John Pisa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi, Juni 26, 2022. Kulia kwake ni Askofu Pisa na kushoto kwake ni Askofu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kujenga mustakabali wa nchi yetu.

ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Juni 26, 2022) katika ibada ya kusimikwa kwa Askofu Mteule Wolfgang Pisa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi katika viwanja vya Ilulu, Lindi.

“Maendeleo ya nchi hayawezi kuimarika kama tutakuwa wabinafsi. Tukiimarisha ushirikiano na ushirikishwaji wa kila mtu, tutaleta maendeleo ya Taifa letu kwa haraka.”

Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na dini zote katika kukuza ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii ili kuimarisha maisha ya kila Mtanzania na Taifa kwa ujumla.

Amesema kwa kuzingatia hayo, Serikali imekuwa ikishirikiana na sekta binafsi zikiwemo taasisi za dini katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini kazi na majukumu makubwa ya viongozi wote wa dini.

Mheshimiwa Majaliwa amesema miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na kuwaongoza watu kiroho kwa kuwapa mafundisho, kutoa ushauri na kuwajenga kiimani.

“Vilevile, mmekuwa mkiwasaidia watu katika shida mbalimbali hususan wale wenye uhitaji kama yatima na wajane sambamba na kutoa ushauri nasaha na malezi bora kwa vijana.”

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga akitoa salamu za baraza hilo amesema Kanisa Katoliki limeahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika masuala yote ambayo Serikali imekusudia kuyafanya kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Rais huyo wa TEC ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya amesema hivi sasa kanisa hilo linawahamasisha waumini wake kushiriki katika zoezi la Sensa Watu na makazi litakalofanyika Agosti 23, 2022.

Askofu Nyaisonga ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iendelee kuliunga mkono kanisa hilo katika shughuli mbalimbali linazozifanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo ikiwa ni pamoja na suala la elimu na huduma nyingine za kijamii.

Naye, Askofu Pisa baada ya kusimikwa amewashukuru wana-Lindi ambao wamempokea na kuonesha umoja na ushirikiano bila ya kujali madhehebu yao, hivyo amesema hatua imempa moyo na imani kwamba atafanyakazi kwa kushirikiana na wananchi wote.

Amesema kwa sasa jamii imevamiwa na utandawazi ambao umepokelewa na watu wengi na kuleta athari kubwa kiimani, utamaduni na mila, hivyo kuchangia mmomonyoko wa maadili hususani kwa vijana. “Nawaomba Watanzania wenzangu tubaki katika mila na utamaduni wetu wa asili na tusizolewe na upepo wa utandawazi.”

Post a Comment

0 Comments