Ticker

6/recent/ticker-posts

UWT NJOMBE YAVIOMBA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUONGEZA NGUVU KUPAMBANA DHIDI YA UKATILI


*************

Na Mwandishi wetu, Njombe

JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake was Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe imeviomba vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani humo kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto ambayo yanaendelea kuongezeka katika mkoa huo.

Hayo yamebainishwa na wanawake wa Jumuiya hiyo kwenye mkutano wa mwenyekiti wa UWT mkoa wa Njombe Bi,Skolastika Kevela na baadhi ya wajumbe,viongozi na madiwani katika halmashauri ya mji wa Makambako uliofanyika katika ofisi za Chama hicho tawi la Ubena mjini humo.

Lucy Mbogela na Magreth Mfilinge ni miongoni mwa wajumbe waliotoa kilio chao dhidi ya matukio hayo huku wakibainisha kuwa katika halmashauri hiyo tatizo hilo limekuwa ni kubwa na kubainisha kuwa ndani ya miezi mitatu pekee kumeripotiwa kesi 57 za unyanyasaji.

“Kuna tatizo kubwa la unyanyasaji wa wanawake na watoto,ukienda kituo cha polisi pale ni foleni ya kesi za unyanyasaji na wanawake wale wanakosa msaada wa kisheria mpaka unakuta unyanyasaji hauishi”walisema wanawake

Aidha katibu wa jumuiya hiyo mkoa wa Njombe Bi,Rehema Mbwana ametoa wito kwa maafisa ustawi wa jamii kushirikiana zaidi na jamii pamoja na jeshi la polisi kitengo cha dawati la jinsia ili kuongeza mapambano dhidi ya ukatili.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoa wa Njombe Bi,Scolastika Kevela ameonyesha kusikitishwa na kulia pamoja na wanawake hao huku akiomba jamii kubadirika na kuwataka wanawake kuongeza kasi ya kujitafutia uchumi binafsi kwa kuwa matukio mengi ya ukatili huo yamekuwa yakijitokeza kwa wanawake na watoto wao kutokana na utegemezi.

“Hii inasikitisha sana lakini niwaase kina mama tumiliki uchumi,tukimiliki uchumi baadhi ya matukio kwenye maeneo yetu yatapungua lakini Njombe ni matajiri wa Parachichi,mtu ukiwa na ekari moja huangaiki hata kidogo,niwasisitize tuhakikishe tunapata angalau ekari moja ya parachichi”alisema Bi,Kevela.

Mwenyekiti huyo ameendelea na ziara yake katika halmashauri ya Makambako mara baada ya ziara hiyo kuifanya katika halmashauri ya Wanging’ombe na Ludewa huku ikiwa lengo lake ni kukutana na kuzungumza na viongozi wa jumuiya hiyo katika halmashauri zote za mkoa wa Njombe

Post a Comment

0 Comments