Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI GEKUL: TUMEJIPANGA KUENDELEZA MASHINDANO YA UTAMADUNI KILA MWAKA


***************************

Na Eleuteri Mangi, WUSM-Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amefungua mashindano ya Utamaduni yanayohusisha ngoma na vyakula vya asili kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na kuhimiza mashindano hayo kufanyika kila mwaka.

Mashindano hayo yamefunguliwa Julai 1, 2022 jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Uhuru ambapo Mhe. Gekul amewaeleza wananchi kuwa wizara hiyo haina jambo dogo, hivyo wamejipanga vyema kuendeleza mashindano ili yafayike kila mwaka kwa mzunguko mikoa yote.

“Leo ni siku ya kipekee, hili ni tukio la kihistoria, ni mara ya kwanza tamasha hili la kitaifa kuandaliwa, tamasha la mwaka huu ni mwanzo wa kufanyika kwa matamasha haya nchi nzima kwa kuzunguka mikoa yote, muioneshe dunia kuwa Tanzania ni tajiri wa Utamaduni na umahiri wake” amesema Mhe. Gekul.

Aidha, amesisistiza kuwa kumalizika kwa tamasha la mwaka huu, ni mwanzo wa maandalizi ya tamasha la mwaka 2023 na mikoa itajulishwa mapema ili mashindano hayo yaanzie ngazi ya kata, wilaya, mkoa na hatimaye yafanike kitaifa.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kufungua mashindano hayo, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu amesema Tamasha la Kwanza la Utamaduni la Kitaifa ambalo linaendelea katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, Julai 2, 2022 litaanza na matembezi ya kiutamaduni katika jiji la Dar es salaam ambayo yatapokelewa na Mhe. Kassim Malaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia atazindua rasmi tamasha hilo.

Ameongeza kuwa Julai 3, 2022 wizara hiyo imeandaa usiku wa taarabu ambao umebeba sura ya kimataifa kwa kuhusisha vikundi vya taarabu kutoka nchi za Burundi, Kenya na Visiwa vya Comoro.

Post a Comment

0 Comments