Ticker

6/recent/ticker-posts

NSSF YAWAHIMIZA WAJASIRIAMALI KUCHANGAMKIA FURSA KWA KUJIUNGA NA MFUKO HUO


NA MWANDISHI WETU, SABASABA

WAJASIRIAMALI wadogo na wa Kati wanayo nafasi kubwa ya kujenga maisha yao ya sasa na ya baadaye kwa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii NSSF, Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi wa Mfuko huo, Bi. Rehema Chuma (pichani juu), amesema.

Amesema chini ya Mpango wa Kitaifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Isiyo Rasmi, ni muhimu kundi hilo nalo liingie kwenye Hifadhi ya Jamii ili na wao wanapofika umri ambao hautawawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali waweze kufaidika na Mafao ambayo wenzao waliokuwa kwenye sekta rasmi (ajira rasmi) wanayapata.

Amewataja Wajasiriamai hao walio katika sekta isiyo rasmi kuwa ni wote wanaofanya shughuli za kuwapatia kipato halali na kutolea mfano, Bodaboda, Mamalishe, Machinga, Waendesha bajaji, Mafundi cherehani, Wakaanga chipsi, Saluni za kike na kiume na Mafundi Uashi.

“Tunaposema tunajenga Maisha yako ya Sasa na ya Baadaye, mwanachama atafaidika kwa kupata Mafao mbalimbali mathalan tuna Fao la Uzazi hili litamuhusisha mwana mama ambaye alikuwa mjamzito, Fao la Msaada wa Mazishi na Fao la Mirathi, lakini tuna Fao la Uzee ambalo hili ndio fao muhimu kwa mtu ambaye uwezo wa kufanya kazi umekoma, mfano kwa uzee au maradhi,”alifafanua.

Meneja huyo ambaye alikuwa akiwahamasisha wananchi wanaotembelea Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba kujiunga na Mfuko huo, Julai 2, 2022, amesema ni rahisi sana kujiunga.

“Mwanachama anaweza kujiunga kwenye ofisi zetu zilizoenea kote nchini na kwa wale wanaotembelea Maonesho haya ya Sabasaba tuko banda namba 13, njoo na kitambulisho cha NIDA au Namba, kisha utajaza fomu na kupigwa picha, na papo hapo tutakutengenezea kitambulisho na kuwa mwanachama rasmi wa NSSF.” Alifafanua na kuongeza hata kama mtu hana kitambulisho cha NIDA, bado anaweza kuandikishwa.

Kuhusu viwango vya uchangiaji Meneja huyo alisema kima cha chini cha uchangianji kila mwezi ni shilingi elfu ishirini (20,000/=) lakini anaweza kuchangia zaidi kulingana na kipato chake.

Aidha alisema baada ya mwanachama kupata kitambulisho chake na namba ya uanachama, uwasilishaji michango nao pia ni rahisi,

“Sasa hivi mfumo wa kulipa kupitia simu ndio umezoeleka sana na sisi tunatumia utaratibu huo wa kufanya malipo ya serikali kupitia mitandao ya simu, benki au wakala wa benki.” Alifafanua.

Aliwaondoa hofu wajasiriamali hao kuwa hata kama kipato chake wakati mwingine hakimuwezeshi kulipa shilingi elfu 20 kwa mkupuo, anaweza kuchangia kidogo kidogo kama shilingi elfu 2,000/=, 5,000/= na kuendelea kupitia namba maalum ya malipo aliyopewa (control Number) ilimradi inapotimia mwezi mwanachama awe amekamilisha malipo ya shilingi elfu 20,000/= kwasababu Mfumo unatambua kiwango hicho cha chini cha uchangiaji kwa mwezi.
Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi wa Mfuko huo, Bi. Rehema Chuma amesema (katikati), akimpatia elimu na kujibu mwaswali kutoka kwa mjasiriamali huyu (kulia) aliyetembelea banda la Mfuko huo Julai 2, 2022.
Bi. Rehema Chuma (kulia), akibadilishana mawazo na Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke Bw. Feruzi Mtika kwenye banda la Mfuko huo Julai 2, 2022
Afisa Matekelezo Mwandamizi, NSSF, Bi. Ummy Kimario (kulia), akimuhudumia mwananchi aliyefika kwenye banda la NSSF.
Afisa Matekelezo Mkuu, NSSF, Bi. Asha Salum (kushoto), akimsikliza mwanachama wa Mfuko huo aliyetembelea banda la NSSF ili kuhudumiwa

Post a Comment

0 Comments