Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA AWAAGA VIJANA 16 WANAOKWENDA KUSOMEA MASOMO YA SAYANSI AFRIKA KUSINI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amewaaga vijana 16 watakaokwenda kusomea masomo ya sayansi na teknolojia katika Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.

Akizungumza leo Januari 30, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ofisi za Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Prof. Mkenda amesisitiza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza idadi ya wataalamu wa sayansi na teknolojia nchini, hususan katika nyanja za Data Science, Akili Unde na Allied Sciences.

Mpango wa Samia Scholarship Extended unalenga kutoa fursa kwa wanafunzi bora wa Kitanzania waliopata ufaulu wa juu katika Kidato cha Sita, hasa kwenye masomo ya sayansi ikiwemo Advanced Mathematics.

Prof. Mkenda amesema wanufaika wote 50 wanatoka shule mbalimbali za kata, serikali na binafsi, jambo linaloonyesha kuwa fursa hii inatolewa kwa wote wenye uwezo bila kujali asili ya shule au familia.

Ameongeza kuwa Baada ya kundi la kwanza, serikali imepanga kupeleka wanafunzi wengine 34 katika vyuo vya kimataifa vilivyoko Ireland Kaskazini.

Aidha ameeleza kuwa Tanzania inahitaji wataalamu wengi zaidi katika nyanja za sayansi na teknolojia ili kuendana na kasi ya maendeleo ya dunia.

Prof. Mkenda alisisitiza kuwa teknolojia ni matokeo ya matumizi ya sayansi, hivyo serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuandaa wataalamu kupitia programu ya Samia Scholarship Extended.

"Mpango huu unalenga kuongeza idadi ya wataalamu wa fani muhimu ikiwemo Data Science, Artificial Intelligence, Allied Sciences na Sayansi ya Nyuklia, ambapo wanafunzi wa shahada ya kwanza na uzamili wanapatiwa ufadhili wa masomo ndani na nje ya nchi". Amesema 

Prof. Mkenda amebainisha kuwa kuanzishwa kwa ufadhili wa masomo ya Sayansi ya Nyuklia ni kutokana na uwepo wa madini ya urani nchini na umuhimu wake katika tiba na kilimo.

Amesema kuwa tayari wanafunzi wa shahada ya uzamili wameanza kusomea fani hiyo nje ya nchi na wanafunzi bora wa shahada ya kwanza watapelekwa kusomea nje ya nchi katika vyuo vikuu mahiri.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Nombo, amesema serikali itaendelea kuwekeza kwenye programu za kimkakati kama Samia Scholarship Extended DS/AI, kwa kuwa zinasaidia kujenga msingi wa maendeleo ya muda mrefu kupitia sayansi na teknolojia.

Profesa Nombo amewataka wanafunzi kuzingatia kuwa wao ni mfano kwa vijana wengine waliopo mashuleni, na kwamba nafasi hizo zinapatikana kwa misingi ya ushindani wa kitaaluma (merit-based), hivyo wanafunzi wajitahidi katika masomo hasa ya sayansi na TEHAMA.

Amesema uwepo wa taasisi kama Nelson Mandela Institute of Science and Technology umechangia kwa kiasi kikubwa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kitaaluma na maisha, ikiwemo financial management na stadi za karne ya 21.

Mmoja wa wanufaika wa programu hiyo, Malaika Florence, amesema mafunzo ya awali waliyopata kupitia boot camp yamewajengea uwezo mkubwa katika masuala ya usimamizi wa fedha, matumizi ya teknolojia na kujiamini katika mazingira ya kimataifa.

Amesema awali wengi wao walikuwa hawana ujuzi wa msingi wa matumizi ya kompyuta, lakini sasa wamejifunza stadi za kisasa ikiwemo uandishi wa codes, matumizi ya lugha mbalimbali za programu kama Python na Java, pamoja na mbinu za kujifunza kwa kujitegemea.

Malaika ameongeza kuwa wamejifunza pia sera za uhamiaji, namna ya kuishi na watu wa tamaduni tofauti, pamoja na umuhimu wa kujenga mitandao ya kitaaluma, akisisitiza kuwa “maisha ni watu” na mafanikio yanahitaji ushirikiano.

Naye Aswile Simon, ambaye amepata nafasi ya kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha programu hiyo, akisema pasipo uongozi wake vijana wengi wasingeweza kupata fursa adimu kama hiyo.

Aswile amesema wanafunzi wanatambua imani kubwa waliyopewa na Taifa, hivyo wana wajibu wa kusoma kwa bidii na kurejea nchini wakiwa na maarifa yatakayosaidia kuendeleza sekta ya teknolojia, uchumi wa kidijitali na ubunifu.

Sambamba na hayo wanafunzi wote nchini wameaswa kuchangamkia masomo ya sayansi na teknolojia, huku serikali ikiombwa kuendelea kupanua wigo wa programu za ufadhili wa masomo ili kuzalisha wataalamu wengi watakaoliwezesha Taifa kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu.

Post a Comment

0 Comments