Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI NA WAFANYABISHARA MAZINGIRA BORA ZAIDI ILI KUIMARISHA UWEKEZAJI NCHINI.


*****************************

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah anayeshughulikia Viwanda na Biashara kwa niaba ya Waziri wa Uwekezji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameshiriki hafla ya Uzinduzi wa bidhaa zenye chapa ya MIDEA nchini Tanzania.

Hafla ya uzinduzi wa bidhaa zenye chapa ya MIDEA zinazotengenezwa na kampuni ya Sichuan Kairui International Co. Ltd ya nchini China imefanyika tarehe 23 Julai, 2022 katika ukumbi wa hoteli ya Serena iliyopo jijini Dar es salaam.

Dkt. Abdallah amesema kuwa Dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ili kukuza uchumi wa nchi yetu, kuboresha maisha ya Watanzania katika kutoa ajira kwa wananchi na kuongeza mapato kwa serikali.

Dkt. Abdallah ameishukuru kampuni ya Sichuan Kairui International Co. Ltd kwa juhudi zao za dhati za kuunga mkono serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza dhana ya uwekezaji nchini kwa vitendo.

Dkt. Abdallah ameongeza kuwa serikali imetenga maeneo ya uwekezaji ya kutosha katika Mikoa yote hivyo niwaombe kampuni hii kuanzisha kiwanda cha kuunganisha bidhaa (Assembling Plant) za MIDEA badala ya kuagiza bidhaa kamili kutoka China.

Dkt. Abdallah amesema kuwa serikali imeendelea kuboresha miundombinu wezeshi ikiwemo reli ya kisasa (Standard gauge), ufanisi wa utoaji mizigo bandarini, ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa ndege Dar es salaam na uboreshaji wa Viwanja vya ndege Mikoani, kuwekeza katika upatikanaji wa nishati ya gesi na umeme wa uhakika mjini na Vijijini, Ujenzi wa Bwala kubwa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha umeme wa MV 2115 kwa mwaka.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Kampuni ya Sichuan Kairui International Co. Ltd nchini Tanzania Bwana Emanuel Metta ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa juhudi zinazoendelea za kuboresha mazingira ya uwekezaji iliyopelekea uwekezaji mkubwa kufanywa katika nchi yetu ambapo kampuni kupitia chapa ya MIDEA inayotengeneza bidhaa mbalimbali za majumbani vikiwemo Viyoyozi, Vichemsha maji, soketi, swichi za umeme,

Bwana Emanuel Metta ameongeza kuwa kampuni ya Sichuan Kairui International Co. Ltd imepanga kujenga kiwanda nchini Tanzania cha kutengeneza vipuri kwa kiwango cha kimataifa kabla ya mwaka 2025.

Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Sichuan Kairui International Co. Ltd Bwana Li Ming amesema kuwa kampuni kupitia chapa ya MIDEA nchini Tanzania imeajiri wafanyakazi 58 ambapo ajira za kudumu ni 45 na wafanyakazi wa mkataba ni 13.

Bwana Ming ameongeza kuwa kampuni imeshirikiana na wadau mbalimbali katika usambazi na ufungaji wa bidhaa zenye chapa ya MIDEA nchini ikiwemo Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Kampuni ya AZAM, Sea Cliff Hotel, TBA, JWTZ na taasisi mbalimbali ambazo zimepelekea kuongeza ajira na kampuni pia inashiriki katika utoaji wa mafunzo kwa wadau na wateja wa namna ya utuimiaji wa bidhaa za MIDEA.

Post a Comment

0 Comments