Ticker

6/recent/ticker-posts

VIFARANGA VYA KUKU KUTOKA NJE YA NCHI MWISHO JULAI 30

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), akizungumza kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma na kuweka wazi kuwa baada ya tarehe 30 mwezi huu, hakuna vifaranga vya kuku vitakavyoingizwa hapa nchini kutoka nje ya nchi na kwamba serikali haitoi tena vibali vya kuingiza vifaranga hivyo ili kuzuia ugonjwa mafua ya ndege na kulinda wazalishaji wa vifaranga wa ndani ya nchi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Stephen Michael ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko akizungumza kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma ambapo amesema katika Mpango Kabambe wa Sekta ya Mifugo wa Mwaka 2016 umefanya tathmini na kuainisha kuwa hadi kufikia Mwaka 2031 kutakuwa na upungufu wa nyama kwa tani milioni 1.8 hivyo tasnia ya kuku ni rahisi ikitiliwa mkazo itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa nyama nchini. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo Bw. Evance Ntiyalundura akiwa kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku jijini Dodoma ambapo amefafanua hatua mbalimbali katika kukuza tasnia hiyo ikiwemo ya kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na wadau wa tasnia. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga, akiwa mmoja wa washiriki katika kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma na kuelezea umuhimu wa wadau kujisajili kwenye mfumo ili kutambulika kisheria na namna serikali inavyotoa vibali mbalimbali vya kusafirisha mifugo kikiwemo cha kuku. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rweguza akifafanua umuhimu wa matumizi ya vyakula bora vya mifugo hususan vya kuku na kuwakumbusha wazalishaji wa vyakula hivyo kutumia maabara ya Wakala ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuhakiki ubora wa vyakula wakati aliposhiriki kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Dkt. Daniel Mushi akitolea ufafanuzi ombi la wafugaji wa kuku kuwepo kwa machinjio ya kuku kila wilaya ili kuzuia uuzwaji holela wa kuku na kuwepo kwa bei elekezi ya kuku sokoni, wakati aliposhiriki kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Katibu wa Chama cha Wadau wa Kuku Tanzania (PAT) Bw. Manase Mrindwa akielezea changamoto za chakula cha kuku kuwa kumetokea ongezeko la bei ya chakula cha kuku hadi kufikia Shilingi Elfu 80 kwa mfuko mmoja kwa mwezi wa Julai kutokana na ongezeko la bei ya mahindi na mashudu ya soya kwenye soko la Tanzania pamoja na kuelezea uwepo wa uhaba wa vifaranga, wakati akisoma taarifa ya chama hicho kwenye kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Muonekano wa washiriki katika kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo kimejumuisha menejimenti ya wizara Sekta ya Mifugo, wazalishaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na wafugaji wa kuku ambapo wametoa maoni mbalimbali ya namna ya kuboresha tasnia hiyo na kuomba kuwepo kwa vikao vya namna hiyo mara kwa mara lengo likiwa ni kukuza tasnia. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


*************

Na. Edward Kondela

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema baada ya tarehe 30 mwezi huu, hakuna vifaranga vya kuku vitakavyoingizwa hapa nchini na kwamba serikali haitoi tena vibali vya kuingiza vifaranga hivyo.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (22.07.2022) jijini Dodoma wakati wa kikao cha wizara na wadau wa tasnia ya kuku, kujadili namna ya kukuza tasnia hiyo ambapo lengo la hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria ya mwaka 2006 ambapo serikali imekuwa ikizuia uingizaji wa vifaranga nchini kutoka nje ya nchi ili kudhibiti ugonjwa wa mafua ya ndege kwa mifugo jamii ya ndege na kulinda wazalishaji wa kuku ndani ya nchi.

Akizungumza wakati akifunga kikao hicho kilichojadili ajenda mbalimbali zikiwemo za upatikanaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na bei ya kuku sokoni, Mhe. Ulega amesema ni mategemeo kuwa serikali haitaona vifaranga vinaingizwa nchini kutoka nje ya nchi na kutaka kuwepo kwa mfumo wa taarifa zinazohusu wazalishaji wa vifaranga vya kuku kuanzia wazalishaji wakubwa hadi wadogo ambao wamesajiliwa na kutoa taarifa serikalini ili kuiwezesha kujua kiwango cha uzalishaji na kuwa na takwimu sahihi juu ya mahitaji ya vifaranga nchini.

“Ni mategemeo yetu ni kutokuona baada ya tarehe 30 mtu anaingiza vifaranga hapa nchini kutoka mahali popote pale, jambo la pili kuwepo na mfumo ambao utasaidia serikali kujua ni kiasi gani cha uzalishaji vifaranga ndani ya nchi yetu ili kujipima uwezo wetu na mahitaji yetu ndani ya nchi.” Amesema Mhe. Ulega

Awali Naibu Waziri Ulega akizungumza wakati akifungua kikao hicho cha wizara na wadau wa tasnia ya kuku amesema tasnia hiyo imekua kwa kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na kuwepo kwa soko linalotokana na ongezeko la watu na kipato, ongezeko la uwekezaji na uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji katika tasnia ya kuku, urahisi wa kufuga kuku na uwezekano mkubwa wa kuwamiliki kuliko wanyama wakubwa.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Stephen Michael akizungumza kwenye kikao hicho amesema kutokana na umuhimu wa tasnia ya kuku katika Mpango Kabambe wa Sekta ya Mifugo wa Mwaka 2016 umefanya tathmini na kubainisha kuwa hadi kufikia Mwaka 2031 kutakuwa na upungufu wa nyama kwa tani milioni 1.8 hivyo tasnia ya kuku ni rahisi ikitiliwa mkazo itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa nyama nchini.

Bw. Michael ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema ufugaji wa kuku ni njia rahisi na ambayo haihitaji maeneo makubwa na miundombinu mingi tofauti na mifugo mingine hivyo kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kimeunganisha wadau wa tasnia hiyo pamoja na kutatua changamoto zilizopo kwa kuzingatia uwepo wa taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo kwa vijana na akina mama na vikundi mbalimbali ambao wengi wamejizatiti katika biashara ya kuku.

Naye Katibu wa Chama cha Wadau wa Kuku Tanzania (PAT) Bw. Manase Mrindwa amebainisha changamoto za chakula cha kuku kuwa kimefikia hadi Shilingi Elfu 80 kwa mfuko mmoja kwa mwezi wa Julai ambapo kunatokana hasa na ongezeko la bei ya mahindi na mashudu ya soya kwenye soko la Tanzania.

Bw. Mrindwa amebainisha pia changamoto ya kutokea kwa uhaba wa vifaranga kwa wakati fulani wa mwaka, huku mitaani bado viko vifaranga visivyo bora ambavyo vinawafikia wafugaji hususan wafugaji wadogo.

Kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kimejumuisha menejimenti ya wizara Sekta ya Mifugo, wazalishaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na wafugaji wa kuku ambapo wametoa maoni mbalimbali ya namna ya kuboresha tasnia hiyo na kuomba kuwepo kwa vikao vya namna hiyo mara kwa mara lengo likiwa ni kukuza tasnia hiyo kwa kuirasimisha na kuwepo kwa machinjio maalum kwa ajili ya kuku na bei elekezi ya kuku sokoni.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments