Ticker

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI WA SHAMBA LA MKONGE KIBARANGA WAHAKIKISHIWA MALIPO YAO YA MWAKA 2017.


***********************

Na Hamida Kamchalla, MUHEZA

ZAIDI ya sh milioni 202 zimeidhinishwa kwa malipo ya waliokuwa watumishi na walinzi wa mali za shamba la Mkonge la Kibaranga lililopo kijiji cha Kibaranga Wilaya ya Muheza mkoani Tanga ambayo walikuwa wanadai tangu mwaka 2017.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona aliyasema hayo juzi jijini Tanga ambapo pia alizungumzia madai hayo ambayo Wizara ya Fedha iko kwenye hatua ya mwisho ya ulipaji.

Kambona alisema malipo hayo yanajumuisha wafanyakazi wote katika mashamba ambayo yapo maeneo ya Kibaranga sh milioni 128.8, Mivumoni sh milioni 31.8 na Azimio sh milioni 41.7.

“Rais Samia Suluhu Hassan amesikia kilio chenu na tayari fedha zenu zipo zimeshatolewa Wizara ya Fedha zipo kwa Msajili wa Hazina kwa ajili ya malipo ya walinzi wa Kibaranga, Mivumoni na Azimio,

“Nadhani ninyi wote ni mashahidi kuna timu ilikuja kufanya uhakiki wa majina ya wale ambao wanadai fedha zao serikalini lilikuwa ni deni la muda mrefu sana tangu mwaka 2017 na mimi nimekuja ofisini nimelikuta, ilishindikana katika awamu hizo lakini awamu ya sita Mheshimiwa Rais ameidhinisha fedha hizi zitoke na mtalipwa,” alisema.

Aidha alisema baada ya mawasiliano na Hazina ambao wanakamilisha uhakiki wa malipo hayo lakini pia imeonekana kuna baadhi ya watu hawana akaunti za benki kwa hiyo walikuwa wanajaribu kuangalia utaratibu mwingine zaidi wa namna gani ya kupata hayo malipo baada ya kuwa wamefanya uhakiki.

Aidha, Kambona alisema katika uhakiki huo pia ilionekana kuna watu wengine si waajiriwa wa mwanzo na wengine ni vibarua ambao wamerithi kazi hizo kutoka kwa wazazi wao.

“Sasa kuhusu hayo yote watakuja wenyewe wataalamu kutoka Hazina na tumekubaliana kwamba mwisho wa mwezi huu au mwanzoni mwa Agosti watakuwa wameshaanza taratibu za malipo,

“Kwa hiyo niwatoe wasiwasi serikali yenu ya awamu ya sita ni serikali sikivu fedha zenu zimetoka na zipo muda wowote zitalipwa baada ya wao kujiridhisha na uhakiki wao wa taarifa zenu na kwa wale ambao hawana akaunti kuna utaratibu wa kufunguliwa akaunti utatolewa,” alisema Kambona.

Kutokana na hatua hiyo, Kambona aliwaomba watumishi hao kuwa wavumilivu kwani fedha zao zimeshafikia hatua nzuri na ulipaji utafanyika kwa kila mmoja ambaye anastahili atalipwa stahiki zake

“Awali tulikuwa tunapambana kule Hazina lakini kwa kasi ya Waziri wa Fedha hataki kuona madeni madeni haya ndiyo maana haraka sana fedha zimetoka Wizara ya Fedha ziko kwa Msajili Hazina wakikamilisha uhakiki mnalipwa fedha zenu au kama watazipitishia Bodi ya Mkonge basi tutawajulisha ni namna gani tutawafikishia fedha zenu,” alisema.


Athumani Luwuchu ni mmoja wa wafanyakazi katika shamba la Kibaranga tangu mwaka 2005 akiwa mlinzi wa mali katika shamba hilo, alisema kutokana na ukiritimba uliojitokeza hawajalipwa tangu mwaka 2017 hadi sasa lakini anashukuru kwa kauli ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TSB, kuwa watalipwa hivi karibuni.

“Tunaishukuru serikali yetu kwa kutukumbuka katika madai hayo na Mkurugenzi wa Bodi ametuhakikishia kuwa fedha zetu hizo Hazina wameanza kufanya tathmini na watatulipa kuanzia Agosti mwaka huu,” alisema.

Naye Hassan Selemani mlinzi wa mali za Bodi ya Mkonge Shamba la Kibaranga tangu Septemba mwaka 2017 alisema "tunaishukuru serikali kwa kufikia makubaliano ya kutulipa madai yetu hayo tumeambiwa kuanzia mwisho wa mwezi huu wa Julai hadi Agosti tutakuwa tumeshaanza kulipwa”.

Shamba la Kibaranga liko katika Wilaya ya Muheza, kata ya Pande Darajani mkoani Tanga likiwa chini ya usimamizi wa Bodi ya Mkonge baada ya jalmashauri ya Wilaya ya hiyo kushindwa kuliendesha na hivyo kurudishwa kwa Bodi ya Mkonge Tanzania.

Post a Comment

0 Comments