







(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
**************************
NA EMMANUEL MBATILO, PWANI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungana na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amemtaka muwekezaji wa viwanda wa kampuni ya Sino Tan (Kibaha Industrial Park Ltd) kwa ajili ya Kongani ya viwanda kufika katika ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuhakikisha Mpango Mkakati wa Tathimini ya Athari ya Mazingira unafanyika katika eneo la viwanda.
Ametoa agizo hilo leo Julai 1,2022 mara baada ya kufanya ziara katika eneo ujenzi wa viwanda mkoani humo ambapo ameipongeza uwekezaji unaofanywa na kampuni hiyo katika eneo hilo.
Amesema licha ya kampuni hiyo kuwa na mkakati mzuri kwenye uwekezaji wa viwanda wilayani Kibaha basi kuna umuhimu wa taratibu wa kuhakikisha anafahamu ni namna gani wanaweza kujipanga kuhakikisha awaathiri mazingira katika shughuli ambayo watakuwa wanafanya.
"Kwa muktadha wa mazingira kwenye eneo hili, inatakiwa ifanyike Mpango Mkakati wa Tathimini ya Athari ya Mazingira, hili ni andiko kubwa ambalo litasainiwa kwenye ofisi yangu, kwakuwa kuna mambo mengi yanakuja huku ni lazima SEA ikamilike haraka iwezekanavyo". Amesema Waziri Jafo.
Aidha Waziri Jafo ametoa maelekezo ndani ya mwaka mmoja Mpango Mkakati wa Tathimini ya Athari ya Mazingira uwe umekamilika ili kuruhusu michakato mingine iiweze kufanyika vizuri katika mazingira yaliyopangwa vizuri katika eneo hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Kongani ya Viwanda Kibaha ya Sino Tan, Bw. Janson Huang, amemuwakikishia Waziri Jafo kutekeleza maagizo yote waliyowaelekeza ili kuhakikisha uwekezaji ambao wanaufanya unakidhi matakwa na sheria ya Uhifadhi na utunzaji wa mazingira katika eneo hilo.
0 Comments