Ticker

6/recent/ticker-posts

CCM YAKEMEA TABIA YA BAADHI YA WATUMISHI WA HALMASHAURI KUKWAMISHA MIRADI YA MAENDELEO KWA KUTAKA RUSHWA 'TEN PACENT'.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akitazama mitambo katika kiwanda cha kuchakata asali wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mkoani humo. (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).

Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka, Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Sikonge waliohudhuria mkutano wakati wa Ukaguzi wa maendeleo ya Upanuzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo

Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka Akizungumza na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kwa Njia ya Simu wakati akitatua Changamoto ya Ukosefu wa Huduma ya Maji kwa wananchi wa kata ya Tumbi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka, akisoma moja ya mabango ya Wananchi waliofika katika ziara ya ukaguzi wa Kiwanda Nyuzi Mkoani Tabora


Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg. Shaka Hamdu Shaka, Akifurahi wakati akizungumza na Wananchi, katika ziara ya ukaguzi wa Kiwanda Nyuzi Mkoani Tabora.

********************

Na Mwandishi Wetu, Sikonge

CHAMA Cha Mapunduzi (CCM) kimekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa halmashauri nchini kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa sababu ya kutaka ‘Ten Pacent’ (rushwa) kutoka kwa wakandarasi, hali inayosababisha miradi kutokamilika au kufanyika.

Akizungumza jana na wananchi wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema Chama kinafuatilia kwa karibu mwenendo wa baadhi ya watumishi hao wanakwamisha miradi ya maendelo kwa kutaka rushwa kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo.

“Tumekuja kukagua uhai wa Chama chetu na utekelezaji wa Ilani, Chama chetu ndicho kimeunda Serikali, nichukue fursa hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za maendeleo, anazopeleka kwenye wilaya mbalimbali ikiwemo hii ya Sikonge. Sasa fedha nyingi zilizoletwa ziendane na kasi za utekelezaji wa maendeleo endelevu ambayo Rais ameelekeza yafanyike kupitia miradi ya kimkakati.

“Bahati nzuri Rais Samia anajua na anafahamu mahitaji ya wanachi anawaongoza, kwa hiyo kila wilaya na kila Mkoa ametoa vipaumbele na kipaumbele cha kwanza ni huduma za afya kwa jamii na ndio maana hata Wilaya ya Sikonge kwenye hospitali hii ya Wilaya Rais ametoa Sh. bilioni mbili.

“Sasa ujenzi huu wa miradi hii mikubwa ya maendeleo uendane na utoaji bora wa huduma kwa wananchi, majengo haya ambayo yanajengwa , vitendea kazi ambavyo vinawekwa, kwa sababu lazima niseme jambo moja ambalo rais amelifanya anajenga majengo na wakati huo huo analeta na vifaa tiba,” alisema Shaka.

Aliongeza kuwa katika historia ya nchi hii, Rais Samia amekuwa wa kipekee kwani huko nyuma majengo yalikuwa yanajengwa baadae yanabaki kuwa mazalia ya ndege, lakini leo hii wanajenga na wanaweka vifaa vya kisasa, niwaombe wauguzi, madaktari pamoja na wote ambao mnahusika kwa njia moja ama nyingine katika kutoa huduma za afya kwa wananchi lazima wawe rafiki kwa wateja wao.

“Lazima mtengeneze mazingira bora ya kuhakikisha huduma hizi ziendane na kasi ambayo Rais wetu amekuwa akiionesha , bahati mbaya sana na kwa masikitiko makubwa na hili naomba niseme kwenye baadhi ya wilaya ikiwemo hii ya Sikonge kwenye miradi hii ya maendeleo kasi ya uendelezaji na ukamilishaji miradi sio nzuri.

“Haifurahishi kabisa kasi , fedha zinakuja kwenye halmashauri lakini kasi ya ukamilishwaji wa miradi na uanzishwaji wa miradi imekuwa ikisuasusa jambo hilo sio nzuri ,spidi ya Rais Samia kwenye miradi ya maendeleo ni kubwa mno.Sasa panapotokea sehemu pakalegalega , mambo yakawa yanaenda kama ambavyo hatukuyatarajia Chama hatuwezi kufunga funga maneno na hatuwezi kukaa kimya,”alisema Shaka.

Aliwaomba waliopewa dhamana ya katika Serikali watimize wajibu wao wa kumsaidia Rais Samia kutektekeleza yale aliyoyakusudia kwa wananchi badala ya kuwa sehemu ya wakwamishaji.

“Kwenye hili sitafungafunga maneno halmashauri ya Sikonge itabidi mjitathimini na mambo hayaendi vizuri , wako maofisa wamekuwa ni sehemu ya ukwamishaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo, haiwezekani miradi hii inakwama wakati mwingine kwasababu ya wakandarasi kuombwa rushwa iliyokithiri ili ndio wakamilishe hii miradi.

“Taarifa tunazo na tunawajua wanaofanya haya tunawajua , narejea tena taarifa tunazo baadhi ya watumishi wa halmashauri mjitathamini mnachokifanya sio sahihi.Sababu moja ya kukwama miradi hii isianze kwa wakati, sababu moja ya miradi hii kutokamilika kwa wakati baadhi ya watumishi wa halmashauri mnataka cha juu kikubwa , mnawakwamisha wakandarasi,”alisema.

Shaka alisema kwa hiyo wanaposema shughuli za maendeleo zinasuasua na haikamiliki kwa wakati kuna watu wanakwamisha, na hivyo ameomba TAKUKURU wafanye kazi yao na wakitaka CCM inaoneshe njia watawaonesha kwani wanafahamu yanayofanyika.

Aliwataka watendaji waliokabidhiwa dhamana katika halmashauri kuhakikisha wanawafikia waanchi katika maeneo wakiwemo wa vijijini ili kuwasikiliza na kutatua shida zao ambapo ametoa mfano wilayani Sikonge kuna baadhi ya maeneo wananchi wanalalamika kutofikiwa watumishi.

“Tumsaidieni Rais Samia kuwafikia wananchi kutatua kero zao na changamoto zao, ndio jukumu tulilopewa, tusipofanya hivyo itakuwa sehemu ya kukwamishana na mambo hayataenda vizuri,” alisema.UDHALILISHAJI KINGONO

Katika hatua nyingine Shaka alitumia nafasu hiyo kukemea tabia ya udhalilishaji inayodaiwa kufanywa na baadhi ya watumishi waliopewa dhamana katika halmashauri mbalimbali ikiwemo ya Sikonge.

“Nataka niseme na hili la udhalilishaji wanawake kingono, nimelikuta Kaliua na lipo Sikonge, lakini hata kwenye maeneo mengine kwa watumishi wa umma, ujumbe umefika, wenye hiyo tabia waache, waache kuwadhalilisha dada zetu, waache kuwadhalilisha mama zetu, waache kuwadhalilisha ndugu zetu wa kike hapa Sikonge, hiyo tabia imeshamiri kwa sababu tu kuna mtu anadhamana, ana fursa ya kuwasaidia wengine.

“Hamuwasaii mama zetu, hamsaidii dada zetu mpaka muwadhalilishe kingono, Chama kinafuatilia kwa karibu sana, hataturahusu udhalilishaji wa aina yoyote kwa wanawake ndani ya nchi hii, wanawake hawa wanauwezo mkubwa sana katika kufungua fursa za maendeleo katika taifa letu.

“Wakithubutu akina mama wanaweza, hatuwezi kuacha uthubutu wao kwa sababu tu sisi akina baba baadhi yetu tunashindwa kuzuia hisia zetu, tena sio kushindwa kuzuia hisia zetu ila hatuna adabu tu, ni utovu wa adabu tuliokuwa nao,” alisema.

Post a Comment

0 Comments