Ticker

6/recent/ticker-posts

CHONGOLO AKAGUA JENGO LA ICU PANGANI, ASEMA M 900 KUBORESHEA MAZINGIRA.




**************

Na Hamida Kamchalla, PANGANI.

HOSPITALI ya Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga imetengewa sh milioni 900 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira yawe safi na rafiki kwa wananchi watakaofika kupata huduma za afya.

Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameyasema hayo wakati alipofika kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) linaloendelea kujengwa katika hospitali ya Wilaya hiyo ikiwa ni moja ya ziara yake aliyofanya mkoani hapa.

Chongolo amesema katika mipango ya serikali mojawapo ni kuhakikisha inaendeleza uboreshaji katika hospitali za zote za Wilaya nchini ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali za majimbo ambazo zitasaifia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

"Kazi yetu siai chama chenye dhamana, kwanza ni kuhakikisha tunaendelea kuboresha mazingira ya kufanyika kazi na taarifa ya bajeti mwaka huu mnaletewa fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira haya kiasi cha sh milioni 900 lengo ni kuwa na hospitali ya Wilaya yenye hadhi inayofanana na Wilaya yenyewe" amesema.

Aidha alitoa pongezi kwa wauguzi na madaktari wa hospitali hiyo kwa kuwajibika ipasavyo katika kutimiza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi huku akiwataka waendelee kuiweka bidii kwenye kazi na kuwa Wazalendo.

"Niwapongeze kwa kasi kubwa mnayofanya, najua mara nyingine mnafanya kazi zaidi ya muda mnaotakiwa kufanya, lakini mnafanya kwa mapenzi ya wananchi mliopewa dhamana ya kuwatumikia, kuwahudumia, kujali na kulinda afya zao, mnafanya kazi kwa uzalendo, hongereni sana" amesema.

Naye Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya hiyo Dkt. Maulid Majala amesema ujenzi wa jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu limejengwa kwa kutimia fedha za Uviko 19 kiasi cha sh milioni 250 ambapo awali jengo Hilo halikuwepo na inapotokea dharura wagonjwa wanapelekwa katika hospitali ya rufani ya Mkoa Bombo.

"Ujenzi wa mradi huu upo katika hatua ya umaliziaji, ambayo ni sawa na asilimia 80 ya ujenzi wote, kiasi cha fedha kilichotumiia hadi sasa ni takribani sh milioni 167.7 na sh milioni 82.3 zipo kwenye utaratibu wa malipo kwa wazabuni waliotoa vifaa vya ujenzi pamoja na garama za ufundi" amesema.

Majala amebainisha matatizo yaliyojitokeza katika ujenzi huo ambazo zinesababisha kupanda kwa makisio ya ujenzi kwa garama za utekelezaji wa mradi ni pamoja na kupanda kwa garama za vifaa vya ujenzi lakini pia mabadiliko ya michoro ya jengo yaliyotolewa na serikali.

"Baada ya ujenzi wa mradi huu kukamilika tunatarajia kuhudumia wagonjwa watano hadi kumi kwa siku, hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wa rufaa kutoka hospitali ya Wilaya kwenda Mkoa, tunatoa shukrani kwa Rais wetu wa awamu ya sita kwa kutoa fedha za kufanikisha mradi huu" amesema Majala.

Baadhi ya wananchi wilayani humo wameishukuru serikali kwa kuwapeleka miradi mikubwa na kupitia jengo wanalojengewa hali ya kupeleka wagonjwa hospitali ya nje ya Wilaya itakuwa mwisho kwani wamepoteza ndugu wengi kwa kutokuwa na chumba cha uangalizi katika hospitali hiyo.

"Tunaishukuru Rais Samia Sulluhu Hassan kwa makubwa anayotufanyia katika Wilaya yetu, mbali na jengo Hilo pia ametuletea Barabara ambayo itatusaidia kwa mambo mengi, na kufunguliwa uchumi katika Wilaya yetu" amesema Mwanaidi Omari, mkazi wa Majengo

Post a Comment

0 Comments