Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKARANI 8440 WA SENSA NA WASIMAMIZI WENGINE WAMEANZA KUNOLEWA MKOANI TANGA


***************************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.


JUMLA ya makarani 8440 wa sensa ya watu na makazi mwaka 2022 Mkoa wa Tanga wameanza mafunzo yao katika ngazi ya Wilaya yanayotolewa kwa lengo la kuwawezesha kukusanya takwimu sahihi kutoka kwa wananchi.

Mratibu wa sensa ya watu na makazi mkoani humo Tony Mwanjota amesema mafunzo hayo yaliyoanza jana pia wapo wasimamizi wa maudhui 842, na wasimamizi wa tehama wapatao 245 pamoja na watendaji kata 245 na wote wamehidhuria katika vituo vya kazi walivyopangiwa.


Mwanjota alifafanua kwamba katika kila halmashauri ya Mkoa wa Tanga imewekwa vituo vinne vya mafunzo, huku akisisitiza kuwa, "mafunzo haya yanalenga kuwawezesha makarani kwenda kukusanya takwimu ambazo zitatakiwa kujazwa kwenye madodoso" amesema.


"Watu wanasema tunakwenda kuhesabu watu, lakini siyo hivyo tu bali tuna takwimu nyingi ambazo tumekusanya ambazo zitakwenda kutusaidia katika kupanga mipango ya maendeleo yetu, tutaanza kufanya sensa ya watu kwa siku sita, na baada ya hapo tutajua kukusanya takwimu za majengo kwa siku tatu" amesema Mwanjota.


Aidha Mwanjota akitoa wito kwa makarani hao, "kikubwa wazingatie wanachofundishwa ili waelewe na kuweza kwenda kukusanya takwimu sahihi" amesema.


Kwa upande wake Mratibu wa sensa jiji la Tanga Juma Mkombozi amesema katika jiji hilo kuna vituo katika shule ya sekondari Galanos yenye washiriki 388, sekondari Usagara washiriki 440, sekondari Mkwakwani washiriki 250 na sekondari ya Ufundi Tanga washiriki 370, huku wakiwa na watendaji kata 27.


"Mafunzo yameanza vizuri, tumepokea vifaa vya mafunzo jana na leo mafunzo yanaendelea, tunatengeneza ndani ya siku 19 mafunzo yatafanyika kwa nadharia na vitendo,


"Lengo kubwa ni washiriki wetu wafundishwe namna nzuri ya kwenda kuchukua taarifa kwenye kaya na maeneo mengine, ikiwemo takwimu za majengo na takwimu za huduma za jamii katika ngazi ya mtaa" amesema


"Kwahiyo kwetu sisi tunashukuru mpaka sasa hatuna tatizo lolote lililotupata na tunatarajia kila kifaa kitafuia kwa wakati ili mafunzo yafanyike kama ambayo yamepangwa kwenye ratiba yake" amebainisha.


Mkombozi amesema elimu na hamasa vinatolewa kupitia njia mbalimbali kama Vyombo vya habari, mikutano ya hadhara kwenye ngazi ya jamii, lakini pia wanatumia vikao vya kisheri na visivyo vya kisheria kadhalika wanatumia wasanii kueneza elimu ya sensa.


"Kwahiyo kila eneo ambalo ni fursa kwetu tunalitumia, lengo ni kuhakikisha watu wote wanapata elimu, tunachoamini ikifika Agosti 23 kila mtu katika jiji la Tanga atakuwa amepata elimu na atakuwa tayari kushiriki kwa namna ambavyo elimu imemfikia" amesema.


Amefafanua kwamba pamoja na wananchi kujiandaa kuhesabiwa lakini pia watoe ushiriniano kwa makarani watakapofika katika kaya zao siku itakapofika kwani ushiriki wao ndiyo utakaosaidia serikali kupata takwimu sahihi ambazo ndizo zitakakuwa msingi wa ugawaji wa rasilimali za serikali katika kuleta maendeleo.


Naye Ofisa mtendaji wa kata ya Pongwe Erika Njana kupitia mafunzo hayo wameweza kufahamu umuhimu na maana ya sensa na kwamba viongozi wa kata wanali jukumu kubwa kuhakikisha sensa inafanikiwa kwa kushirikiana na kamati za kata na mitaa na wengineo.


"Lakini kupitia sensa, nimeona kabisa kwamba bila kuwashirikisha viongozi hawa wa chini, itakuwa ni ngumu, kwahiyo sisi tutakwenda kushirikiana moja kwa moja na viongozi wetu kule chini kuhamasisha jamii kushiriki sensa kikamilifu" amesema.

Post a Comment

0 Comments