Ticker

6/recent/ticker-posts

IJA YATOA MAFUNZO KWA WATUMISHI WAPYA WA  MAHAKAMA 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo alipokuwa akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa Waajiriwa wapya wa Mahakama ya Tanzania yanayofanyika leo tarehe Mosi Agosti, 2022 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Washiriki wa wakifuatilia zoezi la Ufunguzi wa Mafunzo wa elekezi. 

Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka akitoa neno la ukaribisho katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama.



Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Elia Baha akitoa neno la utangulizi katika zoezi la ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Mahakama.

***************************

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Waajiriwa wapya wa Mahakama kufanyanchini kubadili fikra hasi kwa kuwa na fikra chanya ili kuondokana na utoaji wa huduma kwa mazoea na badala yake watoe huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Akizungumza na Watumishi hao leo tarehe mosi Agosti, 2022 mjini Lushoto wakati akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa waajiriwa hao, Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, Mahakama inatekeleza programu za maboresho yanayomlenga mwananchi. Kwa hivyo, kipaumbele ni kuhakikisha Mahakama inatoa huduma bora zitakazofanya wananchi kuwa na imani na chombo hicho cha haki pamoja na kuwaweka wananchi kuwa karibu na Mahakama.

“Kwa dhamira hii, Mahakama inatutaka sote kwa pamoja kubadilika fikra zetu ili kuondokana na kutoa huduma kwa mazoea na badala yake kupitia mafunzo haya mnaelekezwa kuwa kila mmoja wenu katika nafasi yake ahakikishe anadhamiria kuunga mkono juhudi hizi za Mahakama kwa kwenda kutoa huduma bora kwa namna ambayo itawafanya wananchi na jamii kwa ukumla kuwa na imani nanyi na imani kwa Mahakama,” amesema Mtendaji Mkuu.

Prof. Ole Gabriel, amewaeleza pia Watumishi hao kuwa tayari kufanya kazi kwenye maeneo watakayopangiwa bila manung’uniko kwa kuwa ndiko wananchi wanataka kupatiwa huduma.

“Ni matarajio yangu kuwa mtakubaliana na vituo mtakavyopangiwa kwa kuwa huko ndiko kunakohitaji huduma zenu na ndio maana Serikali ilitoa kibali muajiriwe. Niwadokeze tu hapa kuwa, hakuna sehemu nzuri wala mbaya ndani ya Mahakama na badala yake kila Mahakama ipo kwenye maeneo ambayo wananchi wanaishi,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.

Amebainisha kuwa, Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo katika maeneo ambayo ni ya msingi katika kuwaandaa kuwa watumishi wema wenye haiba, tabia, mienendo na maadili ya kimahakama.

Akizungumzia suala la matumizi ya TEHAMA mahakamani, Mtendaji Mkuu amewaeleza Watumishi wao kulipa kipaumbele suala la matumizi ya teknolojia kwakuwa ndio Mahakama inapojielekeza kwa sasa.

“Mtakapokuwa mnajifunza hapa, mtaelezwa kuhusu mifumo mbalimbali ya KITEHAMA ambayo itatumika katika kuboresha utoaji haki na huduma mbalimbali katika Mahakama. Lengo la kuelekezwa hayo ni kuwataka mfahamu kuwa matumizi ya TEHAMA si hiari bali ni jambo la lazima kwa kuwa mtakutana na mifumo ya kiteknolojia na matumizi yake katika kutoa huduma za kimahakama na kugundua kuwa imeshika kasi katika kila kona ya Mahakama,” amesisitiza Mtendaji Mkuu.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu amesema kwamba, lengo kuu la mafunzo hayo ni kubadilisha mitazamo ya Watumishi wapya ili iendane na mitazamo ya Mahakama hatimaye kuwawezesha kufanya kazi inavyotakiwa.

“Kama tunavyofahamu Watumishi hawa wametoka mazingira tofauti tofauti, wamelelewa katika mazingira mbalimbali pamoja na mitazamo tofauti, kwahiyo lengo kubwa la mafunzo haya ni kuwaandaa ili waweze kuendana na kile ambacho Mahakama inatarajia,” amesema Bi. Patricia.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yamehusisha Watumishi wa Kada za Afisa Utumishi/Tawala, Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani, Maafisa TEHAMA, Maafisa Ugavi pamoja na Madereva.

Mafunzo hayo ambayo imeelezwa kuwa yatakuwa endelevu kwa Waajiriwa wapya wa Mahakama, ni mwendelezo wa Mafunzo yaliyotolewa kwa kundi la Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu yaliyomalizika tarehe 29 Julai, 2022.

Aidha, yanafanyika kwa mara ya kwanza, kwa kuwa kabla ya hapo hakukuwa na mafunzo ya namna hii kwa watumishi hao.

Mada zinazotarajiwa kutolewa katika Mafunzo hayo ni pamoja na Muundo na tamaduni za kimahakama, Mpango Mkakati wa Mahakam ana Mpango wa Uboreshaji Huduma za Mahakama, Huduma kwa wateja, Maadili ya Utumishi wa Umma na wa Mahakama, Ubunifu katika kazi na nyingine.

Post a Comment

0 Comments