Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUENDELEZA MIRADI YA MAENDELEO-MAJALIWA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Ikungi, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida. Agosti 5, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Ikungi, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida. Agosti 5, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Ikungi, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida. Agosti 5, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mradi wa ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Ikungi, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Singida. Agosti 5, 2022.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

****************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuendelea kutolewa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi wakiwemo na wakazi wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Agosti 05, 2022) alipozungumza na wananchi baada ya kutembelea mradi wa ujenzi kituo cha afya cha Iglansoni akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani Ikungi.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha huduma za jamii zinazotolewa nchini zinakuwa endelevu, hivyo amewataka wananchi hao waendelee kuiamini na kuipa ushirikiano.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, David Silinde amesema kituo cha afya cha Iglansoni ni miongoni mwa vituo vya afya 234 vinavyojengwa nchi nzima kwa lengo la kusogeza huduma za afya kwa wananchi.

Amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa hospitali ya kisasa katika wilaya hiyo. “Mbali na Serikali kutoa fedha hizo pia, Mheshimiwa Rais Samia ameridhia shilingi bilioni 13.348 zitumike kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 667, Ikungi.”

Naye, Mkuu wa mkoa wa Singida, Peter Serukamba amesema anataka mkoa huo uwe wa kwanza kwa wananchi wote kuwa na bima ya afya ili wawe na uhakika wa kupata huduma hiyo, hivyo amewahamasisha wajiunge Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Pia, Mkuu huyo wa mkoa ametumia fursa hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, ambayo inatarajiwa kufanyika nchini Agosti 23 mwaka huu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Murro amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuridhia kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo zikiwemo shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa vituo vinne vya afya ili kusogeza huduma kwa wananchi.

Mkuu huyo wa wilaya ameahidi kwamba ataendelea kushirikiana na viongozi wenzake ndani ya wilaya hiyo kuhakikisha fedha zote za maendeleo zinazotolewa na Serikali zinatumika katika utekelezaji wa miradi husika ili tija iliyokusudiwa ipatikane.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi amesema ujenzi wa kituo hicho cha afya cha Iglansoni kinachotarajia kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi huu umefikia asilimia 98 na umegharimu shilingi milioni 500.

Amesema kituo hicho kinatarajia kuwahudumia wakazi 13,608 wa vijiji vya Iglansoni na Mnyange. Mradi huo unahusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, kichomea taka, jengo la upasuaji, wodi ya mama na mtoto na jengo la kufulia.

Baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya, Waziri Mkuu alitembelea mradi ya ujenzi wa chuo cha VETA na mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ikungi, ambako kote aliweka mawe ya msingi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi Wilaya ya Ikungi wamempongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuwasogezea huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu na maji karibu na makazi yao.

Post a Comment

0 Comments