Ticker

6/recent/ticker-posts

SHEIKH MKOA WA SINGIDA, KATIBU MWENEZI WA CCM WAHESABIWA WATOA KAULI NZITO YA SENSA

Sheikh wa Mkoa wa Singida,Issa Nassoro akihesabiwa na Karani wa Sensa wakati wa zoezi la kuhesabiwa lililofanyika nyumbani kwake eneo la Manguanjuki nje Kidogo ya Manispaa ya Singida jana.
Sheikh wa Mkoa wa Singida,Issa Nassoro, Karani wa Sensa ya Watu wa Makazi akiwa katika picha ya pamoja na familia yake baada ya kuhesabiwa.
Familia ya Sheikh wa Mkoa wa Singida,Issa Nassoro ikihesabiwa katika zoezi hilo.
Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu akihesabiwa wakati wa zoezi hilo.


Na Dotto Mwaibale, Singida



SHEIKH wa Mkoa wa Singida,Issa Nassoro amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu mkoani hapa kuendelea kuwahamasisha waislam kwa kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa ya Watu na Makazi wanaopita kwenye majumba yao kwa ajili ya kuwahesabu.

Nassoro alitoa wito huo jana baada ya kuhesabiwa na familia yake nyumbani kwake eneo la Manguanjuki lililopo nje kidogo ya Manispaa ya Singida ambapo alisema kuwa sensa katika Uislamu inakubalika na ilianzishwa na Mtume Muhammad (SAW) na kuwa kama kutatokea watu wakiipinga wanapaswa kupewe elimu.

“Nitumie nafasi hii kuwaomba Waislam wote mkoani hapa waendelee kutoa ushirikiano kwa makarani wanaofanya zoezi la sensa ya watu na makazi ambayo ni muhimu sana kwa kila mwanananchi na taifa kwa ujumla” alisema Nassoro.

Sheikh Nassoro alisema baada ya kumalizika kwa sensa hii ya kitaifa waislam wote wa Mkoa wa Singida watafanya sensa yao ili kupata idadi yao kwa ajili ya kusaidia kupanga mipango yao ya maendelea ikiwemo ya kujenga, shule, madrasa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa .

“Tutafanya sensa yetu ya kiislam ili tuweze kufahamiana na kuhimizana kufanya michango kwa ajili ya maendeleo mbalimbali hatuwezi kushindwa nitolee mfano kwa waislam 4000 kila mmoja akiamua kuchangia Sh.5000 tu kwa mwezi tutakuwa tumepata fedha za kuanza kujenga hospitali yetu”alisema Sheikh Nassoro.

Aliongeza kuwa , sensa ni jambo jema lenye maana, na katika Uislamu hakuna mahala ambapo hawajazungumza habari za sensa, hata katika vitabu vingine tumesoma vimezungumza habari hizi. Hata Mtume alitumia sensa kujua jeshi lake lina watu wangapi.

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu Akizungumzia Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 baada ya kuhesabiwa pamoja na familia yake alisema ni kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.

Alisema taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali na kupata taarifa za msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi za mipango katika ngazi zote.

Aidha Kaburu alisema umuhimu wa sensa hiyo ni pamoja na kigawio katika kukokotoa viashiria vingine mfano Pato la mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa, Ajira na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi.

Pia alisema umuhimu wa sensa hiyo ni kupata taarifa itakayowezesha serikali kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni muhimu kwa usimamizi wa mazingira na msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa demokrasia.

Post a Comment

0 Comments