Ticker

6/recent/ticker-posts

UHABA WA FEDHA KWA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KIKWAZO KIKUBWA KATIKA UTEKELEZAJI.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akimkabidhi chetu Kaimu Meneja Kanda ya Mashariki wa Shirika la World Vision nchini Samuel Charles, baada ya Shirika hilo kushika nafasi ya kwanza kwa kufanya kazi zake vizuri. Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Pili Mnyema akiongea na viongozi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Ofisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Tanga Glory Maleo akitoa taarifa ya utekelezaji katika mkutano wa mwaka kwa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Tanga.

Viongozi mbalimbali wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali wakifuatilia mkutano.


**************************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
UKOSEFU wa fedha katika Mashirika yasiyo ya Kiserikali umekuwa ni kikwazo kikubwa kwani muda mwingi yanajikuta yakishindwa utekelezaji endapo wafadhili hawana fedha au mradi unaofadhiliwa umekwisha.


Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mashirika hayo juzi katika mkutano wao wa mwaka, Ofisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Tanga Glory Maleo alisema tatizo hilo linatokana na kutokuwepo kwa mtiririko wa fedha.


Maleo amebainisha kwamba licha ya ukosefu wa fedha, kuna tatizo la wataalamu kukosa ujuzi katika uandishi wa miradi ambayo ingeweza kuwapatia fedha za utekelezaji lakini pia wadau ambao ni wamiliki wa Mashirika kutoelewa mwongozo uliotolewa mwaka 2020.


"Kuna tatizo la wataalamu kukosa elimu ya uandishi mzuri wa michanganui ya miradi ambayo inawapatia fedha za utekelezaji pamoja na mwongozo wa uratibu wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali uliotolewa mwaka 2020, haufahamiki vizuri kwa wadau ambao ni wamiliki wa Mashirika hayo" amesema.Aidha Maleo amesema mbali na matatizo ya kifedha Mashirika yameweza kufanikisha utoaji wa elimu mbalimbali kwa jamii na kufanya kampeni za kuzuia Mila na desturi zinazofifisha maendeleo, kama vile kuzuia matumizi ya dawa za kulevya.


Maleo amefafanua kwamba, "mashirika yameweza pia kutoa huduma za kiafya, Kiuchumi na kijamii kwa makundi mbalimbali maalumu yenye uhitaji yaliyoki kwenye jamii zetu pamoja na kupinga vitendo vya ukatili".


Amebainisha kwamba katika Mkoa wa Tanga kuna jumla ya Mashirika 271 yanayofanya kazi, lakini ni 152 ambayo yanatoa taarifa za utekelezaji wa shuhuli zake kwa kipindi cha robo.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba ametoa pongezi kwa Mashirika hayo huku aliwasihi kuendelea kutoa huduma nzuri na kujali maslahi ya wananchi wa Mkoa huo katika halmashauri zote 11 za Mkoa.


Kuhusu utegemezi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mgumba amesema hali hiyo inaweza kusababishwa hatari ya kujipenyeza kwa ajenda nyingine zisizofaa, lakini pia hawana uhuru katika utekelezaji wa miradi yanayopata kwakuwa wanafanya kazi kwa kumuhofia mfadhili.


"Hali hii inafanya Mashirika haya kutekeleza miradi kwa kufuata matakwa ya wafadhili badala ya vipaumbele na malengo ya nchi, na utegemezi huu pia unasababisha kupenyeza ajenda hasi katika mipango ya nchi na miradi kutokuwa endelevu" amesema.


"Lakini pia Mashirika haya mengi yamekuwa yakijielekeza kutoa huduma zake maeneo ya mijini ingawa maeneo hayo hayana matatizo makubwa kama ikilinganishwa na maeneo ya vijijini, hali hii imetokana na wafadhili kuainisha maeneo ambayo kimsingi wako tayari kutoa fedha" ameongeza.


Mgumba amebainisha kwamba baadhi ya Mashirika yamekosa uwazi na utendaji katika uwajibikaji katika utendaji kazi wao kwa kutokutoa taarifa za utekelezaji wa miradi kwa jamii zinazohidumiwa katika ngazi ya mamlaka za serikali za Mitaa na sekretarieti ya Mkoa.


"Kama muongozo inavyoelekeza, hali hii imekuwa ikileta taswira mbaya ya sekta hii miongoni mwa jamii na kufanya mashirika haya kuonekana yanajinufaisha yenyewe kupitia matatizo yanayozikabili jamii tofauti na malengo yaliyokusudiwa" amebainisha.


"Ukosefu wa uwazi pia umesababisha Mashirika kutakatisha fedha haramu, kutumia jina la nchi vibaya na kutoa taarifa zinazopotosha jamii" ameendelea.

Post a Comment

0 Comments