Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWAPA MAWAKILI WAFAWADHI SIKU 14 KUWASILISHA KESI ZILIZOPO

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akizungumza na Mawakili wa Serikali (hawapo pichani) wakati akifunga mkutano wa chama Mawakili hao kilichofanyika jijini Dodoma.Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akizungumza na Mawakili wa Serikali (hawapo pichani) wakati wa kufunga mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika kwa siku mbili jijini DodomaBaadhi ya Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani) wakati akizungumza na Mawakili wa Serikali kabla ya kufunga Mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika Jijini Dodoma.

Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Kigoma, Bw. Allan Shija (aliyeketi mbele katikati) wakifuatilia kwa makini Hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani) wakati akifunga mkutano wa chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara wa taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo mara baada ya kufunga mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali kilichofanyika jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akifuatiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji. Dkt. Eliezer Feleshi.

************************

❖ Mawakili Wajipanga Kuelimisha Umma Kuhusu Katiba na Haki za Binadamu Na Mwandishi Wetu, OWMS, Dodoma

Serikali yawapa Mawakili Wafawidhi wa Serikali siku kumi nne kuanzia leo kuwasilisha orodha ya kesi zilizopo kwenye taasisi za umma wanazofanyia kazi pamoja na majina na vyeo vya wahusika waliosababisha kesi hizo

Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akifunga Mkutano wa Mawakili wa Serikali uliofanyika kwa siku tatu mkoani Dodoma.

Waziri Dkt. Ndumbaro amewataka Mawakili hao kuandaa orodha ya kesi zote za madai zilizo kwenye taasisi zao; chanzo na sababu ya kesi hizo; taarifa hiyo ieleze gharama au hasara ambayo Serikali inaweza ikaingia; na taarifa iseme ni nani amesababisha kesi hiyo kwa jina na cheo chake; na taarifa hizo za kesi ziwasilishwe kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya kipindi cha wiki mbili

“Niwaelekeze Mawakili muwasilishe taarifa hizo za kesi zilizopo kwa kuwa taasisi nyingine zimekuwa ni vyanzo vya kuzalisha migogoro na mhusika aliyehusika kuzalisha mgogoro huo hausiki tena wala kutoa ushirikiano kwa Mawakili kwa kuwapatia taarifa za kutosha kuendesha majadiliano, mashauri, usuluhushi pamoja na kuiwakilisha Serikali mahakamani,” amesema Waziri Dkt. Ndumbaro

Pia, amewaeleza Mawakili wote wa Serikali wajiandae kuelimisha umma kuhusu Katiba tuliyonayo na haki za binadamu ili kujenga uelewa kwa wananchi na kupata hoja zao badala ya kupata hoja kutoka kwa wanasiasa pekee hasa tunapoelekea kuwa na katiba mpya ikizingatiwa kuwa haya ni maelekezo ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi, Chama Tawala kinachoongoza Serikali ya Awamu ya Sita iliyopo madarakani chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Mawakili wake ili wawe na ujuzi na ueledi katika masuala ya mikataba; uchumi wa bluu; haki za binadamu; na uendeshaji wa mashtaka ili kuweza kuendesha kesi kwa weledi na amewaasa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu; maadili; mila, desturi na tamaduni za nchi yetu; misingi ya katiba na sheria za nchi

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewaasa viongozi wa mpito walioteuliwa kuongoza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kuhakikisha kuwa wanalinda imani ya viongozi wa taasisi zao na imani ya wanachama kwa kuongoza chama hicho kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wake badala ya kuwa jukwaa la siasa kwa kuwa Serikali inategemea kupata maoni na ushauri wa kitaalam kutoka kwa wanachama kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu taifa letu

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo amesema kuwa Wizara yake imeyapokea maelekezo ya Mhe. Rais Samia na watayafanyia kazi ili kuratibu utekelezaji wa majukumu ya Mawakili hao ndani ya utumishi wa umma pamoja na kulea Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Post a Comment

0 Comments