Ticker

6/recent/ticker-posts

UDSM YAFUNGUA DIRISHA LA MAOMBI YA UFADHILI WA MASOMO KWA WANAFUNZI

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 3,2022 Jijini Dar es Salaam.

************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

CHUO Kikuu Cha Dar es Salaam kimefungua dirisha la maombi ya Ufadhili wa masomo kwa Wanafunzi kwa kuzingatia viwango vya Juu vya Ufaulu, kwa mwaka wa Masomo 2022/2023.

Ufadhili huu unaotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa jina la University of Dar es Salaam (UDSM) Merit Scholarships.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 3,2022 Jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amesema katika programu hiyo kila mwaka chuo kinafadhili wanafunzi 50 wa Shahada ya awali na wanafunzi 10 wa Shahada ya Uzamili.

Amesema ufadhili huo ni kwa ajili ya vijana wa kitanzania wenye ufaulu wa juu katika mitihani ya masomo ya sayansi kidato cha sita na waliojiunga na shahada za awali na ambao watachaguliwa kujiunga na shahada za Umahiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha Prof.Anangisye amesema Chuo kimetoa ufadhili kwa wanafunzi kutoka Sudani Kusini wanaotaka kusoma shahada ya Awali ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa upande wa wanafunzi walionufaika na ufadhili wa masomo unaotolewa na Chuo hicho wamekiomba Chuo kutoa nafasi nyingi ili watanzania wengi waweze kunufaika na ufadhili huo.

Wamesema ufadhili huo umewasaidia kuweka bidii katika masomo yao kwa kupata alama za juu zilizowasaidia kuendelea kufadhiliwa kwa miaka mitatu.

"Nashukuru chuo kwa kunipatia ufadhili huu kwa sababu wazazi wangu pekee wasingeweza kunisomesha miaka mitatu kutokana na gharama lakini pia umenihamasisha kusoma kwa bidii kulingana na makubaliano kwani unaposhuka chini ya kiwango kilichoweka hauwezi kuendelea kufadhiliwa," amesema Tundui mmoja wa wanafunzi walionufaika na ufadhili huo.

Post a Comment

0 Comments