Ticker

6/recent/ticker-posts

WADAU HAKI JINAI WAPATIWA MAFUNZO UENDESHAJI MASHAURI YA WANYAMAPORI

Na Angel Meela, Mahakama-Arusha

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania pamoja na Taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na uhifadhi wa Mazingira na usalama wa Wanyamapori ‘PAMS Foundation’ kinaendesha mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ikiwepo ujangiri na makosa yanayohusiana na hayo kwa wadau wa haki jinai ili kuwawezesha kuendesha ipasavyo mashauri hayo.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tano (5) jana tarehe 10 Oktoba, 2022 yanayofanyika katika ukumbi wa ‘Palace Hotel’ jijini Arusha, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.Dkt. Paul Kihwelo alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaleta pamoja wadau wa haki jinai na kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo sheria za kimataifa na kitaifa za wanyamapori na ushahidi.

“Mafunzo haya yanatarajia kuwafikia Majaji 15, mahakimu 75, waendesha mashitaka 25 na wapelelezi 25 katika mafunzo kama haya yatakayofanyika sehemu mbalimbali,” alisema Mhe. Kihwelo. Jaji Kihwelo alisema kuwa, katika mafunzo hayo watajadiliana kuhusu vitu gani vya kuboresha kwenye upelelezi hadi hatua ya uendeshaji wa mashauri hayo ili waweze kutenda haki na kuongeza kuwa, changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa mashauri hayo ni pamoja na upelelezi na suala la ukusanyaji wa vielelezo.

“Mafunzo haya yana lengo la kuwaleta pamoja wadau wote na hivyo kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Sheria za kimataifa na kitaifa za wanyamapori na ushahidi, uandishi bora wa hukumu, utoaji wa adhabu, utekelezaji wa amri za Mahakama katika mashauri ya wanyamapori, pamoja na upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na makosa yanayohusiana na hayo,” alibainisha Jaji Kihwelo.

Mhe. Kihwelo alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, uongozi wa Mahakama pamoja na ‘PAMS Foundation’ kwa ushirikiano ambao wameuonesha tangu kuanza kufanyika kwa mafunzo haya.

Aidha; Mkuu huyo wa Chuo aliongeza kwamba, baada ya mafunzo hayo, anatarajia washiriki watakua bora zaidi na pia watakua wametimiza lengo kwani hiyo ndio fursa pekee ya kujadiliana maeneo yote yenye changamoto.

Jaji Kihwelo aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuhusu umuhimu wake na kushiriki kikamilifu huku akimnukuhu Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis kuwa, "Rais Samia Suluhu Hassan alizindua filamu ya 'Royal Tour' lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji na watalii, hivyo kama hatutawalinda ile kazi itakuwa ya bure (Royal Tour) na tutakuwa na athari kubwa kiuchumi hivyo jukwaa kama hili litasaidia kulinda rasilimali ili wageni waje na kuingiza fedha za kigeni."

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mwandamizi na Wakili Mwendesha Mashitaka Kiongozi Mkoa wa Singida, Karen Mrango alisema eneo hilo la wanyamapori kuwa muhimu ni lazima juhudi za wadau zifanyike ili kulinda na kutunza rasilimali zilizopo.

Mafunzo hayo ya siku tano ambayo yamefunguliwa na Mhe. Dkt. Kihwelo ambaye amezindua rasmi mtiririko wa mafunzo ya namna hiyo ambayo yatafanyika pia kwa makundi mengine ya washiriki pamoja na Maafisa wengine, ufunguzi huo umehudhuriwa pia na Bw. Joseph Pande, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka na Maafisa kutoka Mamlaka ya Ngorongoro na TANAPA.

Kundi la kwanza la washiriki litajumuisha Majaji wa Mahakama Kuu, Waendesha Mashtaka Waandamizi na Wapelelezi Waandamizi pekee ambao watashiriki mafunzo hayo jijini Arusha kwa siku tano kuanzia tarehe 10 hadi 14 Oktoba 2022, wakifuatiwa na kundi la pili la Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Wapelelezi ambao watashiriki mafunzo hayo kuanzia tarehe 17 hadi 21 Oktoba 2022. Kundi la mwisho la Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Wapelelezi litashiriki mafunzo hayo katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuanzia tarehe 24 hadi 28 Oktoba 2022.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Maafisa wa Mahakama ya Tanzania wakiwemo Majaji na Mahakimu na watumishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na kadhalika.

Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya ‘IJA’ na ‘PAMS Foundation’ ambayo yalisainiwa tarehe 23 Juni, 2022 jijini Dar es Salaam kati ya Mkuu wa Chuo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ‘PAMS Foundation.’
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori ikiwemo ujangiri na makosa yanayohusiana na hayo kwa wadau wa haki jinai.

Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Makosa dhidi ya Wanyamapori wakimsikiliza Mgeni rasmi alipokuwa akitoa hotuba yake ya ufunguzi.


Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni kutoka Taasisi ya PAMS Foundation, Bw. Samson Kassala akitoa neno kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Bi. Krissie Clarkson wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga akitoa salaam fupi na neno la ukaribisho kwa washiriki wa Mafunzo hayo (hawapo katika picha).Mgeni rasmi ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa Mafunzo hayo. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni kutioka Taasisi ya PAMS Foundation, Bw. Samson Kassala na Washiriki wengine wa mafunzo.

Post a Comment

0 Comments