Ticker

6/recent/ticker-posts

WAHAMIAJI HARAMU KERO KWENYE MAGEREZA NCHINI, MBIONI KURUDISHSA


***********************

Na Hamida Kamchalla, TANGA.


SERIKALI nchini imeahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inawasafirisha wafungwa ambao ni wahamiaji haramu mara tu watakapomaliza kifungo chao ili kuondoa garama kubwa zinazotumika kuwahudumia.


Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Ramadhani Nyamka ameyasema hayo alipofanya ziara yake ya kikazi kukagua miradi ya jeshi hilo pamoja na kuongea na watumishi wa gereza kuu la Maweni, jijini Tanga.


Nyamka amesema serikali inatumia fedha nyingi kuwapa mahitaji yao wakiwa gerezani bila wao kuwa na faida yoyote huku wakiendelea kusababisha shida ambazo zinaizidishia serikali garama mbali na zile za lazima ambazo ni kuwahudumia katika Magereza waliyopo."Wenzetu Kimataifa huwa hawalipendi hili jina lakini sisi kwa lugha yetu ya ndani tunasema ni wahamiaji haramu, kwakweli ni tatizo kubwa, ni mzigo kwa jeshi la magereza, kwa mafungulio ya leo wapo 874 ambao walishatumikia adhabu zao wanasubiria taratibu za usafiri kurudi nchini kwao" amesema.


"Karibu nusu ya gereza ni wao, na kama mnavyojua hawafanyi kazi yoyote hawazalishi, kwahiyo tuna wajibu wa kuwatafuta chakula, ni binadamu Kuna suala la kuugua, inatubidi tuwatafutie chakula, lakini hata wawapo kwenye Magereza ya selo kuna suala la umeme ambao tunabeba sisi mzigo" amebainisha.


Aidha amefafanua kwamba kwa matumizi yote wanayotumia wakiwa gerezani kwa kipindi cha miaka miwili yanagharimu zaidi ya sh bilioni 3 ambazo kama zingeingizwa katika matumizi zingeweza kuboresha miundombinu ya magereza.


"Fedha hizi ni nyingi sana ambazo zingeweza zikaboresha maeneo mengine ya utoaji huduma kwa wafungwa walioko kwa mujibu wa sheria, sasa hii bilioni 3 kwa miaka miwili ni kwa gereza la Maweni pekee, lakini wapo kwenye Magereza mengine nchini ambako wanahitaji kisafirishwa" amesema.


Amebainisha kwamba mbali na gharama wahamiaji hao wamekuwa na usumbufu mkubwa kwa viongozi wa gereza, kuna wakati wanagoma kula hivyo Magereza hawawezi kuwaachia wagome, lakini wakati mwengine inawabidi kutumia juhudi, maarifa na busara kuweza kuwashawishi na kuwarai waweze kula na kuachana na mgomo.


"Lakini inakuwa ni kitu cha muda mfupi, wanaweza wakagoma leo ukatatua baada ya wiki, wiki mbili wakaridi tena kwenye mgomo wao, lakini njia sahihi ya kuondokana na kero hizi ni kuwasafirisha kurudi nchini kwao" amesema.


Aidha amebainisha kwamba wahamiaji hao wanaweza wakasafirishwa lakini inapotokea wahamiaji wengine wameingia nchini hata wale na walikamatwa watakuwa na waliosafirishwa wamerudi tena, hivyo ipo haja ya makusudi kuangalia kuanzia kule wanakotoka kuna tatizo gani na kwa nini wawe wao mara nyingi.


Nyamka ameeleza kwamba wahamiaji hao raia wa Ethiopia ambao ndio wengi wengi kwenye Magereza nchini kuliko nchi nyingine yoyote zinazotuzunguuka inapaswa mamlaka husika kukaa na kutafuta tatizo la wao kuondoka nchini kwao mara kwa mara.


"Kama mamlaka husika hazijakaa zikatambua tatizo hawawezi wakapata ufunbuzi wa kudumu wa tatizo hili, itakuwa ni kila siku tutaendelea kukabiliana nalo" amesisitiza Nyamka.

Post a Comment

0 Comments