-Yaweka msisitizo ushirikishwaji wa Serikali za Mitaa kwenye miradi ya umeme
-Wasisitizwa kutekeleza mradi ndani ya wigo wa mkataba
-Wapewa maelekezo kufanya mradi kwa weledi na utaalamu
-Bilioni 6.6 kuunganisha wateja wa awali 1,929
Morogoro
Wakandarasi wanaotekelza miradi ya kusambaza umeme nchini wametakiwa kushirikiana kwa karibu na Viongozi wa Serikali za Mitaa ili utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme kwa wananchi iweze kuleta tija na kuchochea uchumi wa nchi.
Hayo yamezungumzwa na Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Deogratius Nagu katika kikao maalum cha kwanza cha kufungua mradi wa kuwaunganishia umeme wananchi mkoani Morogoro (Last Milestone Connectivity Project ) ambacho kimehudhuriwa na Wataalam kutoka REA, TANESCO na Wakandarasi kampuni ya Magna Vis Group Ltd.
"Viongozi wa Serikali za mitaa wale ndio wenye maeneo husika na wale ndio watakayoonyesha maeneo tutakayowapeleka wananchi umeme kulingana na wigo uliopo kimkataba na hii itatusaidia sana kufikisha huduma za umeme kwa walengwa wa mradi" Amebainisha Mha. Nagu.
Katika hatua nyingine, Mha. Nagu ameeleza kuwa, mradi huo ni mahsusi katika kutekeleza mpango mkubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuongeza watumiaji wa umeme nchini.
"Serikali imedhamiria kuunganisha takribani wananchi milioni 8.6 kuwezesha kupata huduma ya umeme ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030 ambapo sisi REA tunatekeleza mpango huu kupitia miradi hii ya kuwaunganishia umeme wananchi, " Amesema Mha. Nagu.
Aidha, ameongeza kuwa Mkandarasi atekeleze mradi kwa weledi na kufuata taratibu za kimkataba na hivyo kupelekea mradi kukamilika kwa wakati na kuharakisha wananchi kupata huduma za nishati ya umeme kwa haraka.
Naye, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro Kaskazini, Mha. Zawadi Macha amesisitiza ubora wa mradi kuzingatiwa katika kipindi chote cha mradi na kuhakikisha wanawapa taarifa ya mradi mara kwa mara viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuwawezesha kufahamu hatua mbalimbali za utekelezaji zinazofikiwa.
Vile vile Mha. Msangi ameongeza kuwa, takribani shilingi bilioni 6.6 zimetolewa na Serikali ili kuunganisha wateja wa awali wapatao 1,929 katika Mkoa wa Morogoro kuweza kupata huduma ya umeme na hatimaye kuwawesesha kuendesha shughuli zao za kiuchumi ikiwemo kuchomelea na machine za kusaga zinazotumia umeme.
Halikadhalika Msimamizi wa mradi kutoka kampuni ya Magna Vis Group Ltd, Mha. James Kimaro amebainisha kuwa watazingatia taratibu zote zilizopo katika mradi ili ziende sambamba katika kipindi chote cha utekelezani wa mradi huo mkoani Morogoro.


0 Comments