Ticker

6/recent/ticker-posts

WALIMU 11,396 WAMECHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU YAKIWEMO WAKIWEMO WA UTORO KWA ASILIMIA 66.5



*******************

Na Zena Mohamed,Dodoma.

NAIBU Waziri wa TAMISEMI Festo Dugange ameitaka Tume ya Utumishi ya Walimu kutowafumbia macho walimu wasiozingatia maadili ya kazi ambapo jumla ya walimu 11,396 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na walimu.

Ndugange amesema hayo jijini hapa leo katika mkutano wa kwanza wa Baraza la wafanyakazi wa Tume ya Watumishi wa Walimu Mkoni Dodoma alipokuwa akimuwakilisha Waziri wa TAMISEMI Angellah Kairuki ambapo ametaja jumla ya walimu 7,579 ni watoro sawa na asilimia 66.5.

Huku akisema asilimia zilizobaki ni makosa mengine hivyo ameitaka
Tume ya Utumishi wa Walimu kuendelea kuwaelimisha walimu kutambua wajibu wao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

“Nitoe rai kwa Tume kuendelea kuwaelimisha Walimu kutambua wajibu wao ili waweze kutekeleze majukumu yao kwa weledi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na kwa walimu ambao wanakiuka maadili ya kazi yao msisite kuwachukulia hatua mara moja pale unapopatikana ushahidi usiotia shaka,

“Natumia fursa hii pia kukemea tabia za baadhi ya walimu wanaojihusisha na vitendo visivyoendana na taaluma yao ambavyo vinadhalilisha taaluma ya ualimu,”amesema.

Pia Dugange amewaagiza waajiri na Mamlaka ya Nidhamu kuchukua hatua mara moja pindi kunapokuwa na uthibitisho wa Mwalimu kukiuka Sheria, Kanuni, Taratibu na Maadili ya Kazi ya Ualimu na ya Utumishi wa Umma kwa ujumla,"amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Walimu Paulina Nkwama amesema tume imefanya tathmini kuhusu hali ya walimu nchini ,zoezi hili lililofanywa na Tume kwa kushirikiana na OR – TAMISEMI kwa kutumia Mfumo wa TAMISEMI ujulikanao kama School Information System (SIS).

Ambapo amesema zoezi hilo lilibaini kuwa, mahitaji ya walimu kwa Shule za Msingi ni 298,313, waliopo ni 173,591 na upungufu ni 124,732 sawa na 58%. Aidha, mahitaji ya walimu Shule za Sekondari ni 175,592, waliopo ni 84,700 na upungufu ni 90,892 sawa na 48%. Taarifa hiyo iliwasilishwa kwa Katibu Mkuu OR – TAMISEMI na kuwezesha walimu 9,800 kuajiriwa mwezi Juni, 2022.

"Tume iliratibu na kushughulikia masuala ya utumishi ya Walimu ambapo Walimu 43,322 waliajiriwa,Walimu 41,675 (96.2%) kati ya walioajiriwa, walisajiliwa, Walimu 33,129 (76.5%) walithibitishwa kazini, Walimu 250,905 walipandishwa cheo, Walimu 22,456 walibadilishwa cheo baada ya kujiendeleza kielimu,Walimu 30,773 waliandikiwa vibali vya kustaafu kazi,Mafao ya Walimu 2,282 yanayohusu Pensheni, Mirathi na Mikataba yalishughulikiwa na Tume na kulipwa na Hazina,"amesema.

Amesema Tume ilitoa uamuzi wa mashauri ya nidhamu 11,396 (98.8%) kati ya 11,529 yaliyoanzishwa Katika makosa yaliyotendwa, kosa la utoro limeongoza kwa kuwa na walimu 7,579 (66.5%), makosa mengine tofauti na utoro ni 33.5% ambayo ni pamoja na kughushi vyeti 1,438, mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi 328, ulevi 89 na uzembe 56. Aidha, hadi sasa Tume imefanikiwa kutoa uamuzi wa rufaa za Walimu 991 (95.7%) kati ya 1,036 zilizopokelewa ambapo rufaa 45 zipo kwenye hatua ya uchambuzi ili ziweze kuwasilishwa mbele ya Tume kwa ajili ya kuhitimishwa.

"Pamoja na mafanikio hayo Tume imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi zaidi ya asilimia 40 (Mahitaji 802, waliopo 480, na upunguufu ni 322); Kila ofisi kuwa na msimamizi wa ofisi badala ya Katibu Msaidizi wa Walimu ikiwa ni takwa la kanuni ya 40 ya Kanuni za Tume ya Utumishi wa Walimu za Mwaka 2016,"amesema.

Hata hivyo, Muundo wa Maendeleo ya Utumishi na Mshahara kwa Watumishi wa Tume umewasilishwa OR – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) kwa hatua zaidi.

Post a Comment

0 Comments