Ticker

6/recent/ticker-posts

DKT.TAX AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA URUSI NA IRAN

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini Mhe. Andrey Levonovich Avetisyan wakiwa katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma.

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax akimkaribisha Balozi wa Iran nchini Mhe. Hossein Alvandi Bahineh wakati wa mazungumzo yaliyofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Iran nchini Mhe. Hossein Alvandi Bahineh wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika  jijini Dodoma.

************************

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax leo tarehe 23 Novemba 2022 kwa nyakati tofauti amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini Mhe. Andrey Levonovich Avetisyan na Balozi wa Iran nchini Mhe. Hossein Alvandi Bahineh yaliyofanyika jijini Dodoma. 

Katika mazungumzo hayo mbali na kudumisha na kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia, vilevile yalijikita katika kujadili masuala mbalimbali yenye maslahi mapana kwa pande zote mbili na kimataifa ikiwemo biashara na uwekezaji, utalii, amani na usalama na kuendeleza sekta ya uvuvi na kilimo nchini. 

Dkt. Tax akizungumza na Balozi wa Shirikisho la Urusi nchini Mhe. Andrey Levonovich Avetisyan ameeleza kuwa licha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia uliopo kati ya mataifa haya mawili, Urusi imeendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini. Hivyo serikali itaendelea kudumisha na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo na kuangalia maeno mapya ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kwa upande wake Balozi Avetisyan ameeleza kuwa Urusi itaendelea kushirikiana na Tanzania ikiwemo kuongeza msukumo katika masuala ya uwekezaji, biashara, na utalii. Vilevile aliongeza kusema kuwa katika siku za usoni Urusi inatarajia kuongeza kiwango cha ufadhili wa masomo kwa vijana wa Tanzania kwenda kusoma nchini humo.  

Sambamba na hayo, Balozi Avetisyan alisisitiza utayari wa Urusi kushirikiana na Tanzania katika masuala ya utamadumi ikiwemo kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini humo. Amebanisha juhudi mbalimbali zinazofanywa na Urusi katika kuendeleza lugha hiyo nchini humo, ambapo ameeleza kuwa hadi sasa kuna takriban Vyuo Vikuu vitano vinavyofundisha Kishwahili nchini humo. 

Kwa upande wake Balozi wa Irani nchini Mhe. Hossein Alvandi Bahineh akizungumza na Waziri Dkt. Tax ameeleza kuwa Iran inaingalia Tanzania kama mbia muhimu wa uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku akielezea nia ya Iran ya kuwekeza nchini katika sekta ya kilimo, uvuvi na uendelezaji wa makazi.

Aidha Waziri Dkt. Tax ameeleza utayari wa Serikali ya Tanzania katika kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini. Alieleza kuwa juhudi hizo zinahusisha hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kufanya maboresho ya kanuni, sera na sheria mbalimbali kwa lengo la kuboresha  mazingira ya bishara na uwekezaji nchini. 

Post a Comment

0 Comments